SUAMEDIA

Wafanyakazi na wanafunzi SUA watakiwa kuchangamkia fursa ya udhamini wa masomo nchini India

 Na: Hadija Zahoro

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimepata fursa za masomo na kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa wanafunzi wake wanaotamani kwenda kusoma nchini India.

Udhamini huo unajumuisha Programu mbili ikiwemo ya muda mfupi(ITEC) na Programu ya muda mrefu kwa wale waajiriwa(ICCR) wakijumuisha nyanja ya sayansi ya akili mnemba.

Akizungumza na SUAMEDIA Mei 27,2025, Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya Prof. Esron Karimulibo amesema kuwa ziara hiyo iliyohusisha maafisa wa Ubalozi kutoka nchini India  iliongozwa na Bw.Rajnish Kummar,Mkuu wa Mpango wa ITEC.

Prof.Karimulibo amesema kuwa fursa hiyo haiihitaji kulipia chochote zaidi yakufanya maombi kwa njia ya mtandao na wao watagharamia kuanzia tiketi, pesa ya kujikimu pamoja na pesa ya ada ya masomo mara baada ya majibu kutoka.

‘‘Kwahiyo naahidi mimi ndiyo nimekabidhiwa majukumu na menejimenti kwahiyo nitahakikisha kwamba taarifa hizi zinapatikana kwa wana jumuiya wote’’amesema Prof.Karimulibo.

‘‘Mimi natamani kuona tunachangamikia fursa hizi kwa sababu huwa    bahati haiji mara mbili kwa hiyo tunategemea kwamba kadiri tutakavyokua tunapashana taarifa basi watu wazichangamkie’’ amesema Prof.Karimulibo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mpango wa ITEC, Bw.Rajnish Kummar  amesema kuwa ana matumaini kwa kile walichokijadili kitaleta mafanikio makubwa katika uhusiano wao na SUA zaidi ya uhusiano wa kiuchumi, kifedha na sasa wanaanza kujenga uhusiano huo kwa njia ya udhamini na kuahidi kuwajengea uwezo zaidi kwa kuhakikisha wanapata elimu iliyojitosheleza.

Ameeleza kuwa watakaopata nafasi ya kwenda kusoma nchini India,watafaidika kupata elimu bora zaidi na watapata vyeti ambavyo vitawasaidia kusambaza maarifa yote waliyoyavuna nchini humo kwa watu wengine wakiwemo wanafunzi, wanataaluma pamoja na watu wa kawaida.








Post a Comment

0 Comments