Na: Ayoub Mwigune
Mabalozi
kutoka nchi za Nordic zimeeleza kuridhishwa na mchango wa Taasisi ya SUGECO
katika kuwawezesha vijana na wajasiriamali nchini Tanzania kupitia miradi ya
kilimo na biashara, wakisema ni mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa kimataifa
unaotoa matokeo chanya kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi kutoka nchi hizo, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Jesper Kammersgaard amesema wamefurahishwa na namna maarifa waliyopata watanzania nchini Denmark yanavyotumika kwa vitendo katika shughuli zao za kila siku hapa nchini.
“Tunaona namna ambavyo vijana
waliopata mafunzo kwetu sasa wanatumia elimu hiyo katika kilimo chenye tija, hii
si tu inawasaidia binafsi kiuchumi, bali inasaidia pia maendeleo ya taifa kwa
ujumla,” amesema Balozi Kammersgaard wakati wa ziara ya mabalozi wa nchi za
Nordic katika ofisi za SUGECO mkoani Morogoro.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUGECO Revocatus Kimario, amesema zaidi ya vijana 800 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakiwemo wanafunzi na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wamepata nafasi ya kwenda katika nchi nne kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kupitia ushirikiano na nchi za Nordic.
Kimario ameongeza kuwa vijana hao
wamenufaika kwa kujifunza ujuzi wa kisasa wa kilimo biashara na sasa wengi wao
wameanzisha miradi halisi ya uzalishaji na ujasiriamali kwenye maeneo yao ya
asili, hatua inayosaidia kuimarisha uchumi wa jamii vijijini.
“Hawa vijana si tu wamesafiri
kujifunza, bali wamekuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao, tunatoa wito
kwa vijana wengine waamini kuwa SUGECO ni daraja la mafanikio yao,” amesema
Kimario.
Sweetbeth Komba, mwanafunzi wa Shahada ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya SUA, ni miongoni mwa wanafunzi waliopata nafasi hiyo kupitia programu ya miezi 18 nchini Denmark, amesema alijifunza kwa vitendo kwenye shamba la nguruwe kuhusu uzalishaji, afya ya mifugo na mbinu za kisasa za ufugaji ambazo sasa anazitumia kujitegemea na kusaidia wengine.
0 Comments