Na: Ayoub Solomon Mwigune
Wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo Mkoani Mbeya, wamehimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Kiwele kwa kuhakikisha usafi wa mazingira, vifaa vya kukamulia pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa afya za ng’ombe wao wa maziwa ili kupunguza athari zitokanazo na ugonjwa huo.
Wito huo umetolewa katika mafunzo maalumu yaliyotolewa na Dkt. Benigni Temba, Mhadhiri na Mtafiti wa Mradi wa NANO COM kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kuhusu elimu juu ya ufugaji, mbinu bora za kudhibiti Homa ya Kiwele (mastitis), pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.
Dkt. Temba amesema homa ya kiwele ni ugonjwa unao athiri kiwele cha ng’ombe na kusababisha maumivu, kupungua kwa uzalishaji wa maziwa pamoja na mabadiliko ya rangi na harufu ya maziwa.
Ameeleza kuwa ugonjwa huo upo wa aina mbili, ule unaoonekana wazi kwa dalili kama kiwele kuvimba, kuwa na joto na maumivu, na ule usioonekana kirahisi ambapo maziwa huonekana ya kawaida lakini ubora wake hupungua.
“Homa ya Kiwele husababisha hasara kubwa kwa wafugaji bila wao kufahamu chanzo, hasa pale inapokuwa haina dalili za wazi, ni muhimu wafugaji wakapewa elimu ya kutosha kuhusu utambuzi wa mapema na mbinu sahihi za udhibiti wa ugonjwa huu,” amesema Dkt. Temba.
Amesisitiza kuwa ili kugundua aina isiyo na dalili ya ugonjwa huo, vipimo vya maabara ni muhimu, huku akieleza kwamba homa ya kiwele uathiri ustawi wa mnyama, uongeza gharama za matibabu, upunguza uzalishaji wa maziwa na wakati mwingine husababisha ng’ombe kuchinjwa kabla ya muda au kukataliwa sokoni.
Ameeleza kuwa njia bora za kuzuia ugonjwa huo ni pamoja na kuhakikisha mikono ya mkamuaji na kiwele vinaoshwa kwa maji safi na sabuni kabla ya kukamua, kutumia vitambaa tofauti kwa kila ng’ombe, kusafisha vifaa vya kukamulia kwa maji ya moto na sabuni baada ya matumizi, pamoja na kutenga ng’ombe mwenye maambukizi.
Kwa upande wake, Selestin Samba
Kimaro, Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo amewashukuru
wataalamu kutoka SUA pamoja na mradi wa NANO COM kwa kufanya uchunguzi wa
kiafya kwa ng’ombe waliopo katika Halmashauri hiyo ili kubaini hali halisi ya Homa
ya Kiwele na kusema kuwa elimu iliyotolewa imewafumbua macho wafugaji na
itasaidia kutatua changamoto hiyo kwa vitendo.
Baadhi ya wafugaji waliopata mafunzo hayo akiwemo Fedrick Gaspa na Ally Kitogela wamesema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu udhibiti wa ugonjwa huo na kuwawezesha kuboresha uzalishaji wa maziwa pamoja na kipato kupitia sekta ya ufugaji.
Mradi wa NANO COMM unatekelezwa katika mikoa mitano nchini ambayo ni Tanga, Iringa, Mbeya, Njombe na Arusha ambapo tafiti katika maeneo haya zinalenga kubaini vyanzo vya Homa ya Kiwele na kubuni tiba mbadala kwa ajili ya wafugaji nchini Tanzania.
0 Comments