SUAMEDIA

SUA yatumia Ngamia kukuza uelewa na umahiri wa vitendo kwa wanafunzi

 

Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Tiba za Wanyama na Sayansi za Afya, kimeendelea na juhudi za kukuza uelewa na umahiri wa vitendo kwa wanafunzi wa Ndaki hiyo kwa kutumia Ngamia kama sehemu muhimu ya mafunzo yatakayowasaidia kuwa Madaktari wenye weledi watakapohitimu masomo yao.


Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Stashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji (SUA) wakiwa kwenye jitihada za kumfunga kamba Ngamia ili wamwangushe chini kwa ajili ya kumchoma sindano ya dawa ya minyoo


Hayo yamethibitishwa na Bibi. Enesa Raphael Mlay, Msimamizi wa Shamba la Utafiti katika Ndaki hiyo wakati akitoa mafunzo ya namna ya kuwapa Ngamia dawa za minyoo kwa njia ya sindano kwa Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Stashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji  wanaosoma chuoni hapo.

Bibi. Enesa amesema SUA inaendelea kuboresha ufugaji wa Ngamia kwa ajili ya tafiti, elimu na mafunzo kwa wanafunzi wa taaluma mbalimbali lengo kubwa likiwa ni kuwawezesha wahitimu wa Chuo hicho kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kujiajiri katika fani zao walizosomea.



Bibi. Enesa Mlay (anayemchoma sindano Ngamia) akiwa na Wanafunzi wa Mwaka wa  
 Kwanza wa Stashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji (SUA) akiwaonesha namna ya kumchoma sindano mnyama huyo baada ya kufanikiwa kumwangusha chini  na kumdhibiti


“Ngamia wamekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wetu wanaosomea Tiba ya Mifugo, Sayansi ya Wanyama, Kozi za Ualimu na hata wale wanaosomea  Misitu, ambapo hujifunza namna ya kuwatambua, kuwahudumia na kutambua tabia zao”, amesema Bibi. Enesa.

Amesema mafunzo hayo huwasaidia wanafunzi hao kujiandaa kikamilifu kwa maisha ya kitaaluma pindi wanapomaliza masomo yao kwa kuwa katika shamba hilo la utafiti, wanafunzi hujifunza pia namna ya kushughulika na magonjwa ya Ngamia ukiwemo ugonjwa wa kuharisha ambao ni hatari  kutokana na kusababisha vifo kwa haraka.


Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Stashahada ya Afya ya Wanyana na Uzalishaji (SUA) 
akimchoma sindano Ngamia ikiwa ni sehemu ya mafunzo kwa vitendo huku wenzake wakimtazama


Akizungumzia ufugaji huo, Bibi. Enesa amesema Ngamia ni mnyama wa kipekee mwenye faida nyingi na anayeweza kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo kuwataka wafugaji kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na ufugaji wa Ngamia.

Baadhi ya wanafunzi hao wanaosoma Stashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji akiwemo Marco Lyoba, Zena Maulid, Nicholaus Ruhamvya na zele Emmanuel wamefurahishwa na mafunzo hayo kwa vitendo na kusema yanawajengea hali ya kujiamini kiasi kwamba watakapohitimu watakuwa madaktari wazoefu na hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.






Picha zote na Nicholaus Roman

Post a Comment

0 Comments