SUAMEDIA

Jamii kuzielewa sheria za nchi zinapoandikwa kwa lugha ya Kiswahili kunasaidia kupunguza makosa na utoaji wa haki

Na: Calvin Gwabara - Mwanza

Kukamilika kwa Mwongozo wa Ufasili wa Sheria, Istilahi za Kisheria pamoja na  ufasili wa sheria kuu 446 za Tanzania kutasaidia jamii kuzielewa, kuzifuata na kupunguza kufanya makosa yanayotokana na kutojua kwao sheria sambamba na utoaji wa haki.

Mwandishi Mkuu wa Sheria Bwana Onorius Njole wakati akizindua kikosi kazi hicho maalumu na kushoto kwake ni Mwandishi Mkuu wa Sheria Mstaafu, Bi Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho.

Hayo yamebainishwa na Mwandishi Mkuu wa Sheria Bwana Onorius Njole wakati akizindua kikosi kazi maalumu cha wataalamu wabobevu wa Kiswahili nchini kutoka Chuo Kikuu Huria,Chuo Kikuu cha Dar es salaana, Chuo Kikuu cha Dododma ,Baraza la Kiswahili (BAKITA) na wataalamu wa sheria waliokutanishwa jijini Mwanza kwa lengo la kuhakiki Muongozo wa Ufasili wa Sheria na Istilahi za Kisheria zilizoandaliwa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Mwandishi huyo mkuu wa sheria amesema lengo la Mwongozo huo ni kusaidia kujenga uelewa wa pamoja wa misingi ya ufasili kwakuwa kuna changamoto ya kutengeneza itungo kwa kutumia misamiati ya Kiswahili. Alieleza kuwa wamebaini kuwa wakati mwingine kwenye kutafsiri wanajikuta wanataka kubadili tungo za kiingereza ili zibaki maana ile ile na hivyo kujikuta haieleweki na haibebi yale masharti ya kisheria yaliyopo katika kifungu kilichopitishwa na Bunge. Hivyo Mwongozo huu utawezesha kuwa na mfanano wa tafsiri.

“Tangu nchi yetu ipate uhuru tumekuwa tukitunga sheria kwa lugha ya kiingereza lakini zaidi ya asilimi 80 ya watanzania wanatumia lugha ya Kiswahili kama lugha mama, na tunapotaka kila mtu kufuata sheria maana yake lazima aijue na kuilewa vizuri lakini hawawezi kuilewa kama ipo kwenye lugha ambayo hawaijui huku tukitaka waifuate, hivyo ufasili wa sheria utasaidia sana jamii kupunguza kufanya makosa kwa kujua masharti ya sheria wanayotakiwa kuzingatia haswa kwa kuwa kutojua sheria sio utetezi pale unapofanya makosa” alisema Bwana Njole.

Aliongeza “Kumekuwa na changamoto kwamba utekelezaji wa sheria umekuwa ni mdogo,uzingatiaji wa matakwa ya sheria umekuwa ni mdogo na wakati mwingine sio kwasababu ya ukaidi ila ni kwa sababu ya lugha inayotumika kwenye sheria, hivyo kwa zoezi hili tunalenga kuwawezesha wananchi wazijue sheria na kuzizingatia lakini kusaidia utekelezaji wa sheria hizo na utoaji wa haki”.

Mwandishi huyo mkuu wa sheria amesema Serikali kwa sasa imeweka msukumo mkubwa kwenye kuhamasisha uwekezaji nchini lakini kumekuwa na migogoro kwenye maeneo mbalimbali kati ya wawekezaji na wananchi na ukifuatilia unakuta wananchi hawaifahamu sheria inayosimamia uwekezaji husika hivyo kuna umuhimu wa pande zote mbili kuelewa wajibu wa kila upande kama sheria inavyoelekeza.

Hata hivyo Bwana Njole amesema msukumo huohuo umeelekezwa pia kwenye mahakama za Tanzania kuendesha kesi na kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndio lugha inayoeleweka na watu wengi hivyo mahakama kama chombo cha toa haki lazima ipate sheri kwa lugha ya Kiswahili ili iweze kuzitafsiri vizuri.

Amesema kuwa kufuatia umuhimu huo ni lazima sasa zoezi la ufasili wa sheria lifanyike katika misingi ya ufasili inayofahamika kwa kila mtu na ndio maana wamemua kuandaa Muongozo wa Ufasili ili hata pale mahakama inapokutana na utata kwenye maeneo fulani ya sheria iliyofasiliwa wataweza kutumia muongozo huo kujua misingi iliyotumika kufasili sheria husika yenye utata.

“Pamoja na faida zote hizo lakini kubwa zaidi ni mahakama kutafsiri sheria na kutoa haki kwa Kiswahili katika utoaji wa haki na sheria kwa lugha ya Kiswahili pia kutasaidia kukuza demokrasia,Uchumi, Uwekezaji na maendeleo ya watu kwenye nyanja zote” alibainisha Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho ambaye ni mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari amepongeza jitihada kubwa iliyofanyika katika kuhakikisha kunakuwepo na Muongozo wa Ufasili wa Sheria nchini ili zieleweke kwa maana moja.

Mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho akitoa neno wakati wa uzinduzi.

“Niipongeze sana Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kazi hii kubwa iliyofanyika maana baada ya Serikali kutoa tamko la kila sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili itapelekea watu wengi kujitokeza kufanya kazi hiyo japo kimsingi msimamizi mkuu wa jambo hilo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria” Alieleza Prof. Safari.

Aliongeza “Sasa kufuatia uhitaji huo na watu watakapojitokeza kufasili sheria lazima kuwepo na Mwongozo maalumu wa kuufuata kwenye kufanya kazi hiyo ili kuhakikisha watumiaji wa sheria hizo wanapata maana moja na sio maana tofauti na kuleta mgongano kwenye kutoa haki mahakamani”.

Mdau huyo maarufu wa Kiswahili nchini amesema baada ya zoezi hilo sasa ni muhimu kuwepo kwa kamusi ya sheria na maneno yake kwa lugha ya Kiswahili ili kuweza kutafsiri yale maneno ya kiingereza yanayotumika kwenye sheria na dhana zake kwa Kiswahili fasaha.

Nae Mwandishi Mkuu wa Sheria Mstaafu, Bi Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho amesema kazi hiyo wanayoifanya inaingia kwenye historia kwa kuanda muongozo wa ufasili wa sheria nchini kwakuwa sheria zimekuwa zikifasiliwa kwa utashi wa mtu na sio kwa kufuata muongozo hivyo kazi hiyo wameahidi kuifanya kwa weledi mkubwa ili isaidie kuweka misingi ya ufasili wa sheria na katika utoaji wa haki na uelewa wa sheria kwa kila mtu.

Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihutubia Bunge alisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili. Katika kutekeleza azma hiyo, Mwaka 2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti la kwamba lugha ya sheria sasa ni Kiswahili na lugha ya kutumika katika vyombo vya utoaji haki nchini nay oni Kiswahili

Mwandishi Mkuu wa Sheria Mstaafu, Bi Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mwandishi Mkuu wa Sheria kuzungumza na wajumbe hao.

.

Wajumbe wa Kikosi kazi hicho pamoja na sekretarieti yao kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Bwana Onorius Njole.








Post a Comment

0 Comments