SUAMEDIA

Mradi wa FORLIVES Waimarisha Kilimo na Maendeleo ya Jamii katika Mkoa wa Tanga

 Na: Calvin Gwabara –Tanga.

Mkoa wa Tanga umepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa programu za mafunzo ya jamii (CBT) zinazolenga kuboresha mbinu za kilimo, kuwawezesha wakulima wa ndani, na kuimarisha uwezo wa taasisi mbalimbali na kuchangia kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.

Picha ya pamoja ya wakulima viongozi kutoka vijiji vya Mashindei, Vugiri, Old Ambangulu na Bagamoyo wakati wa mafunzo ya Kilimo Hifadhi na mbinu za kuhimili mabadiliko ya tabianchi Wilayani Korogwe.

Akizungumza kuhusu shughuli na mafanikio ya mradi, Bettie Luwuge, Meneja wa Mradi wa FORLIVES, alisema kuwa mradi huu unahamasisha matumizi yenye usawa ya rasilimali za asili kwa ajili ya maisha endelevu katika Milima ya Usambara Magharibi, Tanzania na kutekelezwa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa ufadhili wa Danmission. Mradi unashirikiana karibu sana na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.

Mradi umejikita kwenye mafunzo na kuijengea uwezo jamii na makundi mbalimbali  umefanya mafunzo kwa wakulima, viongozi wa dini, na maafisa wa kilimo katika wilaya za Korogwe, na Lushoto na kutoa elimu kwa  vitendo, hali iliyochochea maendeleo endelevu katika mkoa huo na uendelevu katia uwakili wa maliasili.

Meneja huyo wa Mradi amesema moja ya mambo muhimu yaliyofanyika ni mafunzo kwa wakulima viongozi (CBT) huko Korogwe katikati ya mwaka jana, yaliyolenga kuwawezesha wakulima kwa mbinu za kisasa za kilimo, uhifadhi wa mazao baada ya mavuno, na uunganishaji wa masoko ambapo washiriki walipata uelewa wa kina juu ya jinsi ya kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, jambo ambalo limekuwa changamoto kwa wakulima wadogo wa eneo hilo.

“Mradi huu pia ulifanya ziara ya mafunzo kwa wakulima viongozi huko Muheza ambao washiriki na kupata fursa ya kuona kilimo cha mazao ya viungo, uhifadhi wa misitu, mnyororo wa thamani wa mazao ya viungo na miradi ya kilimo iliyofanikiwa na kutumia mbinu bora katika maeneo yao, wakulima na maafisa ugani walishirikiana na wataalamu wenye uzoefu na kujadili njia bunifu za kuimarisha ustahimilivu wa kilimo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na wadudu,” alifafanua Bi.Luwuge.

Aliongeza “Mafunzo mengine muhimu yalifanyika Lushoto na yalihusu ujenzi wa uwezo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT- NED) – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo viongozi mahili akiwemo Baba Askofu Msafiri Mbilu (PhD), Sheikhe  Kunguru na wengine kutoka Kamati ya Amani ya Wilaya ya Lushoto ambapo mafunzo yalilenga kuimarisha viongozi wa dini na watumishi wake katika Dayosisi kuhusu Uwakili wa maliasili, kuhimili na kustahimili mabadiliko ya tabia nchi, Iko-Thiologia usimamizi wa migogoro, utawala bora , ushawishi, sera na sheria na namna ya kutumia membari kufikisha ujumbe wa uhifadhi na uwakili wa maliasili kwa jamii”.

Kwa mujibu wa Bettie Luwuge, changamoto kubwa iliyoonekana katika mafunzo yote  ni hali ya matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi yalioathiri mwenendo wa mvua, uwezo mdogo wa kifedha kwani Wakulima wengi wadogo wanakabiliwa na changamoto za gharama na ukosefu wa mikopo.na miundombinu duni katika baadhi ya maeneo imeathiri utekelezaji mzuri wa programu za mafunzo ya kilimo ingawa licha ya changamoto hizo, mafunzo hayo yameleta mafanikio makubwa.

“Wakulima wameripoti ongezeko la uelewa na maarifa kuhusu kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, matumizi endelevu ya ardhi, na usimamizi bora wa mifugo na tayari wengine wameanza kutumia mbinu mpya za kilimo kama vile kilimo cha matuna, mafanya juu fanya chini, kilimo cha mtaro, kuchanganya mazao, kilimo cha kontua, kilimo cha kufunikia mazao, kutotumia moto n.k ili kulinda ardhi, kutunza maji na kupunguza mmomonyoko wa ardhi, jambo lililosababisha mavuno bora na ongezeko la kipato,” alisema Luwuge.

Kwa mujibu wa Bettie Luwuge, ziara ya kujifunza huko Muheza ilionyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali kwa kuwaleta pamoja wakulima, watafiti, na maafisa wa kilimo kwa kuunda jukwaa la kubadilishana maarifa kuongeza hamasa ya kilimo cha mazao ya viungo na mnyororo wa thamani yake katika Wilaya ya Korogwe.

Akizungumzia mafunzo hayo Sheikh Baruti kwa niaba ya viongozi wa dini wa wilaya ya Lushoto amesisitiza hitaji la kuwa na programu za maendeleo zilizopangiliwa vizuri ndani ya taasisi za kidini na umuhimu wa kutumia nafasi zao za uongozi wa dini kuhamasisha miradi ya uwezeshaji wa jamii zaidi ya utoaji wa huduma za kiroho,” alisema Luwuge.

 "Binafsi, nahisi nimepewa jukumu kubwa, maana nahusika kwenye Mpango wa Baraka na Amani katika Baraza la BAKWATA, jukumu hili la kuhamasisha ujuzi tuliojifunza hapa kwa wenzangu ni muhimu ili uweze kuenea kwa waumini wote hivyo nina furaha na nipo tayari kuanza upya."Alisema Sheikhe Baruti.

Kwa upande wake Askofu Joseph Mbilu alisisitiza washiriki wa mafunzo yaliyofanyika Lushoto kuwa hata kazi ianyofanywa na mradi huo ni kazi ya Mungu kwakuwa inawajengea uwezo watu kuweza kufanya kazi na kuzalisha kwa tija ili kujiletea maendeleo.

Baba Askofu DKT. Msafiri Mbilu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT- NED) – Dayosisi ya Kaskazini Mashariki akizungumza kwenye mafunzo hayo.

“Jambo moja kuu ambalo lipo wazi katika maandiko, kwamba tumekosa katika zamani na sasa ni lazima tusimame na tuendelee mbele, Sauti ya Mungu kupitia Yeremia 2:7 inatufundisha: "Nalikuletea katika nchi ya rutuba ili ule matunda yake na mazao yake yaliyojaa; lakini mlijia na kuichafua nchi yangu na kuihatarisha urithi wangu." Warsha hii inapaswa kutuongoza kurudi katika njia sahihi”alisisitiza Askofu MBilu

Aliongeza “Wataalamu wamependekeza uwekezaji mkubwa zaidi katika huduma za ugani na programu za ujenzi wa uwezo ili kuendeleza athari chanya za mafunzo haya hivyo kuna kuna haja ya sera zinazosaidia upatikanaji wa fedha na pembejeo za kilimo kwa wakulima wa vijijini na kupanua mafunzo haya katika wilaya nyingine kutasaidia kufanikisha maendeleo endelevu ya kilimo.”

Meneja wa Mradi wa FORLIVES, Bettie Luwuge, amesema kuwa ili kuendelea mbele, wadau wakiwemo serikali za mitaa, taasisi za kidini, na mashirika ya kilimo wanapaswa kushirikiana ili kupanua miradi hii kwa msaada sahihi na mafunzo endelevu, wakulima na viongozi wa jamii watakuwa na ujuzi wa kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha usalama wa chakula na kuwa na uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika mkoa huo.

Mafanikio ya programu hizi ni ushahidi wa nguvu ya kushirikishana maarifa na maendeleo yanayoendeshwa na jamii kwani kadri maeneo mengi yanavyoanza kutumia mbinu kama hizi, Tanzania itanufaika kwa kuwa na sekta ya kilimo yenye ustahimilivu na yenye tija zaidi.

Mradi wa Uhifadhi wa Misitu, Haki na Maisha Bora kwa jamii (FORLIVES Project), unahamasisha matumizi yenye usawa ya rasilimali za asili kwa ajili ya maisha endelevu katika Milima ya Usambara Magharibi, Tanzania na unatekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa ufadhili wa Danmission katika Vijiji vinne ambavyo ni Mashindei (Kata ya Lewa), Vugiri, Old Ambangulu na Bagamoyo (Kata ya Vugiri), Tarafa ya Bungu Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga


Wakulima kutoka Korogwe wakisikiliza kwa makini hatua muhimu za kufuata wakati wa kupanda mazao ya viungo aina ya pilipili manga kutosha shamba la mkulima mzoefu kijiji cha Mkumba Bwana Ramadhan Hashim Wilayani Muheza.





Washiriki wakijifunza mbinu ya kutumia matuta, mbogamboga aina ya vitunguu, spinachi na kabichi huzalishwa na CBT kwenye mashamba darasa, kijiji cha Bagamoyo, Wilaya ya Korogwe kwaajili  ya kusaidia kuongeza kipato, kulinda ardhi na kupunguza kasi ya kuingia msituni wakati huo huo kuongeza uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.


Kitalu cha miche ya mazao ya viungo aina ya Karafuu na Mdalasini kijiji cha Bagamoyo. Miche zaidi ya 6500 imeoteshwa kwa ajili ya wakulima kupanda mashambani mwao.

Askofu Dr Joseph Mbilu, Dean J Kanju, shekhe Kunguru na viongozi wa Diosisi ya KKKT Kaskazini Mashariki wakiwa na Wakuu wa majimbo, na wachungaji pamoja na watumishi wa Diosisi, mwakilishi wa Danmission na watumishi wa TFCG wakati wa mafunzo ya uwakili wa maliasili-Lushoto.

Post a Comment

0 Comments