SUAMEDIA

BAKITA yapongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kuandika sheria za nchi kwa Lugha ya Kiswahili

Na: Calvin Gwabara – Mwanza.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lapongeza kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kuhakikisha sheria zote za Tanzania zinaandikwa kwa lugha mama ya Kiswahili.



Mhariri Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) bwana Richard Ntambi akitoa salamu za baraza hilo mbele ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (hayupo pichani)

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Mwanza Mhariri Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa bwana Richard Ntambi amesema watanzania wengi wanaelewana vizuri kwa kutumia lugha ya Kiswahili hivyo kuwa na sheria zilizo kwenye lugha yao kutasaidia jamii kuzijua sheria hizo vizuri na kuzifuata tofauti na sasa ambapo zipo kwenye lugha ya kiingereza ambayo wengi wao hawaifahamu.

“Changamoto kubwa iliyopo hasa katika masuala ya haki na mahakama ni matumizi ya lugha ya kiingereza hasa kwa jamii kutoelewa vyema majadiliano yanayofanyika kwenye mahakama hizo na kwenye hukumu zinazotolewa hali inayopeleka malalamiko mengi na wengine kulazimika kutumia gharama kupeleka hukumu zao kwa watu kuwasaidia kutafsiri sheria na hukumu zao hivyo haya yote yatamalizika kupitia kazi hii ya matumzi ya Kiswahili mahakamani” alisema Bwana Ntambi.

Mhariri Mkuu huyo kutoka BAKITA amesema wanatambua changamoto ya uwepo wa misamiati michache ya Kiswahili kukidhi ile ya kiingereza lakini jitihada zinafanyika kuhakikisha kuwa misamiati ya Kiingereza inapata misamiati sahihi kwa lugha ya Kiswahili kwa kutafuta kutoka kwenye misamiati ya makabila mbalimbali nchini na pale inapokwama wanatumia njia ya utohozi wa misamiati hiyo ya kiingereza kwakuwa ni njia pia inayokubalika.

Kwa upande wake Mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari amesema kazi hiyo kubwa na nzuri inayofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imekuwa ni kilio cha muda mrefu cha Watanzania wengi na wadau wa Sheria na Haki.

Mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaaa Wakili na Profesa wa Sheria Prof. Abdalah Safari akitoa salamu zake wa wadau hao wa Kiswahili na sheria nchini

Prof. Safari amesema baada ya kazi hiyo sasa ni muhimu kuwa na kamusi ya sheria kwa Kiswahili ingawa tayari Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imetengeneza Istilahi za Kiswahili ambazo zinatakiwa pia kupitiwa kwa pamoja na wataalamu wa  sheria na lugha ili kujiridhisha na usahihi wake .

“Pamoja na kutengenezwa kwa istilahi hizo za kiingereza kwa lugha ya Kiswahili sasa ni wakati wa kufikiria kitu kikubwa zaidi kama kamusi rasmi ya sheria kwa kiswahili ili kuwezesha hata zoezi la ufasiri kuwa jepesi na kujenga uelewa wa pamoja kwa kila mtu na kila mdau wa sheria” alibainisha Prof. Safari.

Prof. Safari alieleza kuwa Waingereza walitawaliwa na Warumi na kulazimishwa kutumia lugha ya kilatini kwenye sheria zao lakini baada ya kujikomboa wakagundua mtu anafanya vizuri jambo kwa lugha mama hivyo wakabadilisha, kwahiyo na Watanzania lugha mama ni Kiswahili.

“Sheria inasema kutojua sheria sio utetezi lakini kama mimi siijui sheria na nikavunja maana yake siunanionea? Hivyo kuwa na sheria za Kiswahili kutaleta haki kwa watu wote maana watakuwa wanaweza kuzisoma sheria na kuzielewa na kuzifuata” Alifafanua Prof. Safari.

Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria inaendelea kutekeleza maazimio ya Serikali iliyoyatoa Mwaka 2021 kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti kwamba lugha ya sheria sasa ni Kiswahili.

Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini Bwana Onorius Njole akieleza mipango ya Ofisi yake kupitia Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali nchini inavyohakikisha adhma ya serikali ya sheria zote kuandikwa kwa kiswahili inavyotekeelezwa mbele a wajumbe wa kikosi kazi hicho.


MATUKIO KATIKA PICHA NI WATAALAMU WA KISWAHILI NA SHERIA WAKIENDELEA NA KAZI YA KUPITIA MUONGOZO WA UFASILI WA SHERIA.







Post a Comment

0 Comments