Na: Calvin Gwabara – Mwanza.
Katika kuhakikisha kuwa maamuzi
na maazimio ya Serikali ya kutumia lugha ya Kiswahili kwenye kuendesha kesi
mahakamani na katika utoaji wa hukumu, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria tayari
imemaliza kazi ya kutafsiri sheria kuu zote 446 za Tanzania kwa lugha ya
Kiswahili.
Hayo yamebainishwa na Mwandishi
Mkuu wa Sheria nchini Bwana Onorius Njole wakati akizungumza na Kikosi kazi cha
Wataalamu nguli wa lugha ya Kiswahili na
sheria nchini waliokutanishwa na Ofisi yake kwaajili ya kuandaa Muongozo wa Ufasili
wa Sheria unaofanyika jijini Mwanza.
“Tanzania tuna sheria kuu
zipatazo 446, na tunatambua sote kuwa sheria hizo zote zilikuwa zimeandikwa kwa
lugha ya kiingereza lakini baada ya maagizo ya Serikali ya kutaka mahakama
kutumia lugha yetu Mama na sheria kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili tulifanya
kazi hiyo kubwa na nzito lakini tunafurahi sasa kusema kuwa tumeikamilisha na
tuna rasimu ya sheria kuu zote kwa Kiswahili hivyo kupata muongozo huu wa
ufasiri utatusaidia sasa kutumia kupitia rasimu hizo ili ziwe na mfanano pamoja na kuondoa mkanganyiko kabla ya kuanza
kutumika” Alieleza Bwana Njole.
Aidha amesema kuwa baada ya kumaliza
zoezi la urekebu wa sheria toleo la mwaka 2023 na kufanya ufasili wa sheria
hizo wameona itakuwa na maana kubwa kama wataweza sasa kutoa toleo la sheria hizo
zote zilizorekebiwa kwa lugha ya Kiswahili kwa kufuata muongozo rasmi ifikapo
mwanzoni mwa mwaka ujao wa fedha ili ziweze kuanza kutumika.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria
nchini amesema huko nyuma wamekuwa wakifanya ufasili wa sheria kawaida bila
kuwa na chombo maalumu cha kuwaongoza kuhakikisha kunakuwa na mfanano lakini
wanaamini baada ya kuwepo kwa Mwongozo
huo sasa kutawezesha kuandika vizuri sheria kwa Kiswahili na kufasili vyema
zilizopo.
“Kwahiyo Mwongozo huu wa ufasili wa sheria tunauhitaji sana
ili hata inapotokea changamoto kutokana na tafsiri hiyo tunarudi kwenye Mwongozo
kama msingi wa ufasili kuliko hivi sasa ambapo kila mtu anafanya ufasili kwa
kutumia utashi na uelewa wake hali inayoweza kuleta misuguano ya kisheria isiyo
ya lazima na kupotosha maana ya dhana husika.
Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati
akihutubia Bunge alisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi
kwa kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili. Katika kutekeleza azma hiyo, Mwaka
2021 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria
ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti la kwamba
lugha ya sheria sasa ni Kiswahili na lugha ya kutumika katika vyombo vya utoaji
haki nchini nay oni Kiswahili.
PICHANI NI WAJUMBE WA KIKOSI KAZI CHA WAKIENDELA NA ZOEZI LA KUPITIA MUONGOZO WA UFASILI WA SHERIA.
0 Comments