Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Watafiti wanafunzi kupitia mradi
wa AGRISPARK wametakiwa kuhakikisha wanazingatia kanuni na sheria za uandaaji
wa Vitabu vya elimu kwa wakulima ili viweze kusomeka vuzuri na kueleweka na
kila mkulima ili elimu iliyomo iweze kuwasaidia.
Wito huo umetolewa na Msimamizi
wa kitengo cha rejea na huduma za Makataba kwa jamii kutoka Maktaba ya Taifa ya
Sokoine ya Kilimo SUA Bwana Jabir Jabir wakati akifundisha akifundisha timu ya
Wataalamu Wanafunzi wa mradi wa AGRISPARK namna ya kufanya usanifu na uhariri
wa taarifa kwaajili ya kuandaa vitabu vya Elimu Kwa wakulima.
“Wakati mtakapoanza kuandaa vitabu vya elimu kwa wakulima kuhusu
mbinu bora za kilimo na ufugaji, ni muhimu kutumia lugha rahisi na inayoeleweka
kwa wakulima wengi maana lugha inapaswa kuwa fasaha lakini isiyo na maneno
magumu ya kitaalamu yasiyoweza kufahamika kirahisi na wakulima wa kawaida
lakini pia matumizi ya mifano halisi yanayohusiana na mazingira ya wakulima
husika yatawasaidia kuelewa na kuhusisha maelezo na maisha yao ya kila siku,
hivyo kuongeza uelewa na utekelezaji wa maarifa wanayopata” alisema Jabir.
Msimamizi huyo wa kitengo cha
rejea na huduma za Makataba kwa jamii kutoka Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya
Kilimo (SNAL - SUA) amesema muundo wa kitabu unapaswa kuwa wa kuvutia na rahisi
kusomeka, ukiwa na maandishi yaliyopangiliwa vizuri, vipengele vilivyogawanywa
kwa utaratibu, na matumizi ya vielelezo kama picha, michoro na jedwali.
Jabir amesema vielelezo hivyo
vinasaidia kuelezea hatua kwa hatua mbinu bora za kilimo na ufugaji, hasa kwa
wakulima wasiojua kusoma vizuri lakini wanaweza kuelewa kwa kuona na ni muhimu
kuhakikisha kuwa kila sura inajengwa kwa mtiririko mzuri wa maarifa, kuanzia
dhana za msingi hadi mbinu za hali ya juu, ili msomaji aweze kujifunza kwa
utaratibu mzuri.
“Maudhui ya vitabu vinavyohusu
kilimo na ufugaji yanapaswa kuwa sahihi na kuzingatia hali halisi ya mazingira
ya kilimo ya wakulima husika, hii inamaanisha kuwa vitabu vinapaswa kuzingatia
aina ya udongo, hali ya hewa, mbegu bora, mifugo inayofaa, na mbinu za kisasa
zinazotumika katika maeneo husika kwa kuzingatia tafiti za hivi karibuni na
ushauri wa wataalamu wa kilimo na ufugaji zinapaswa kuzingatiwa ili kutoa
taarifa zilizo sahihi na zinazoweza kutekelezeka kwa urahisi na wakulima.
Aidha Jabir amewema vitabu hivi
vinapaswa kuwa na sehemu za maswali na majibu, hadithi fupi za mafanikio ya
wakulima waliotumia mbinu husika, na hata maelezo ya wapi wakulima wanaweza
kupata msaada zaidi.
Kuwashirikisha wakulima katika
uandishi wa vitabu hivi pia ni muhimu, kwani watatoa ushuhuda wa changamoto
wanazokutana nazo na mbinu zilizowasaidia na kwa kufanya hivyo, vitabu vitakuwa
na uhalisia zaidi na vitawafanya wakulima kuviona kama nyenzo halisi za
kuwaongoza katika kuboresha shughuli zao za kilimo na ufugaji.
MATUKIO KATIKA PICHA WASHIRIKI WIKIFUATILIA MAFUNZO.
0 Comments