Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Watafiti wa mradi wa AGRISPARK
kutoka Chuo Kikuu caha Sokoine cha Kilimo SUA wameanza utekelezaji wa mpango wa
uandaaji wa vitabu vidogo vyenye lengo la kutoa majibu ya changamoto mbalimbali
za wakulima nchini kwa kuwapatia mafunzo wanafunzi watafiti watakaoshiriki
kwenye kuandaa vitabu hivyo.
Akifungua mafunzo hayo Mtafiti Mradi
wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa
Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPARK) Dkt.Philbert Nyinondi
amewataka wataalamu hao kuzingatia mafunzo hayo ya awali ambayo yanalengo la
kuwajengea msingi wa kazi hiyo ambayo wanatarajia kuanza kuifanya.
“Kwanza niwapongeze kwa kupata
nafasi ya kushiriki kwenye kufanya kazi hii muhimu kati ya wanafunzi wengi wa
Chuo chetu, Mtambue kuwa kazi hii mnayoifanya ni kwa maslahi ya wakulima na
wafugaji wetu maana vitabu mtakavyoandaa tunatarajia vitasaidia kujibu
changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakulima na wafugaji na vitasambazwa
kwa njia mbalimbali kuwafikia ikiwemo kupitia mfumo wa MKULIMA LIBRARY uliopo kwenye Maktaba ya Taifa ya Kilimo”
alifafanua Dkt. Nyinondi.
Mkuu huyo wa mradi wa AGRISPARK
amesema baada ya mafunzo hayo watapata nafasi ya kwenda kwenye maeneo
mbalimbali ya mradi ikiwemo Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro na
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kwaajili ya kukutana na wakulima na
kuzungumza nao katika mazingira halisi ili kupata taarifa mbalimbali kuhusu
mada za vitabu wanavyoviandaa.
Aidha Dkt. Nyinondi amewataka
kuzingatia mambo mbalimbali wakutanapo na wakulima vijijini ikiwemo swala la
matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kwa kutochanganya na lugha ya kiingereza
kwenye mazungumzo yao,Mavazi, Maadili ya jamii husika pamoja na kutowaona
wakulima kama hawajui bali watambue kuwa wana uzoefu wa miaka mingi na wanajua
vitu vingi ambavyo wao hawajui.
Nae kwa upande wake mtafiti mkuu
mwenza wa Mradi huo wa (AGRISPARK) Dkt. Nicholaus Mwalukasa amesema wakati wa
mafunzo hayo watapitishwa kwenye mada mbalimbali ili kuwajengea uwezo katika
kutekeleza kwa ufanisi zoezi hilo ikiwemo mnyororo wa thamani wa mazao
mbalimbali, Kilimo bora cha mazao, masuala ya masoko, Mbegu bora za kilimo
pamoja na namna ya kuandaa vitabu hvyo.
“Mafunzo haya tumeona ni muhimu
sana kwenu kufanyika kabla ya kuanza kazi kubwa iliyo mbele yenu, na tunaamini
baada ya mafunzo haya na kuelewa upana wa kazi hii na matarajio ya mradi
mtaweza kufanya kazi nzuri ambayo itakuwa na mchango mkubwa kwa wakulima wetu
na taifa kwa ujumla wake” Alisisitiza Dkt. Mwalukasa.
Dkt. Mwalukasa amesema kazi
inayofanyika ni sehemu ya utekelezaji wa wa malengo ya mradi huu ya kutumia Mbinu
Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa
na Teknolojia za Kilimo kwa kutengeneza vijitabu vizuri ambavyo
vitasaidia kufikia lengo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya
washiriki wenzake Hawa Twaibu amewahakikishia viongozi wa mradi huo na SUA kuwa
watafanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanatimiza malengo ya mradi kwa
wakati na kwa ufanisi mkubwa katika kipindi chote watakachukuwa kwenye zoezi
hilo.
“Tunashukuru Mradi wa AGRISPARK
na Chuo kwa kutupa nafasi ya kufanya kazi hii muhimu kwa wakulima wa Tanzania,
na tunaamini kupitia kazi hii itatupatia uzoefu mkubwa kwenye kuteleza mazoezi
ya aina hii siku zijazo na kutusaidia kuweza kujua namana ya kufungasha elimu
na kuifikisha kwa wakulima na wahitaji wengine” Alisema Hawa.
Mradi wa AGRISPARK Ulizinduliwa mwishoni mwa kwama 2024 na Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAs) Dkt. Geofrey Karugila kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda na unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Sokine cha Kilimo SUA kama maono makubwa ya Chuo katika kuinua watafiti wake hasa wachanga kwa kutenga fedha za ndani ili wafanye tafiti za kusaidia kutatua changamoto za jamii na taifa.
Matukio katika picha Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia maelekezo na nasaha za ufunguzi.
0 Comments