SUAMEDIA

Viwavijeshi vamizi wanavyoacha kilio na umasikini kwa wakulima wilayani Mvomero

Na: Calvin Gwabara - Mvomero

Wakulima wa mahindi Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kupitia watafiti wake kutafuta suluhisho la kudumu la namna ya kuwakabili viwavi jeshi vamizi ambao wanaharibu zao la mahindi na kuziacha familia nyingi na njaa na umasikini mkubwa.

Mkulima wa mahindi kutoka kata ya Wami Dakawa wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Salehe Mwendi akizungumza na watafiti wa mradi wa AGRISPARK - SUA.


Wakiongea na watafiti wa mradi wa AGRISPARK – SUA wilayani humo wamesema kila mwaka hali inakuwa mbaya zaidi kutokana na kushindwa kuwadhibiti wadudu hao hatari ambao sasa wanashambulia na mazao mengine yote ya kijani pale mahindi yanapokauka shambani.

Akizungumza kwenye kikao hicho kuwakilisha wakulima wengine Mkulima wa mahindi kutoka kata ya Wami Dakawa wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, Salehe Mwendi amesema kwa sasa kilimo kimekuwa kigumu na changamoto za wadudu na ukame vinatuacha masikini wakulima wengi kwenye maeneo mengi.

“Jamani tunaiomba serikali kupitia watafiti wake na mamlaka zingine zenye uwezo wa kusaidia kupata ufumbuzi wa wadudu hawa, miaka ya nyuma tulizoea ukilima mahindi unasubiria kuvuna lakini kwa sasa hali imekuwa mbaya sana bila kupuliza madawa hupati chochote shambani, tunatumia nguvu kubwa kulima lakini wadudu wanatunyima mazao yetu hasa kwa sisi ambao hatuna uwezo wa kununua madawa” alisema Mzee Mwendi.

Aliongeza “Kwa sasa tunalima shamba tunapanda na kuhudumia kwa kupalilia kisha tunaacha wadudu wale na kile watakachobakisha shambani ndicho na sisi mwisho tunaenda kuokoteza na kurudisha nyumbani kula na familia yetu, maana tulikimbilia kwenye zao la mpunga ambalo nalo haliathiriwi na wadudu hawa lakini sasa kwa miaka mitatu mfululizo ndege wanakuja makundi kama mchanga wakishuka shambani siku moja wanamaliza hata ekari 12, yani tunateseka sana”.

Nae Mkulima mwingine Mzee Mohamed Kigonile ameomba watafiti wa Mradi wa AGRISPARK – SUA kuwa kama kuna elimu sahihi ya kukabiliana na wadudu hao basi waandike vitabu na vipeperushi vinavyoweza kutoa maelekezo sahihi ya namna ya kufanya ili kuokoa mazao yao.

Mkulima wa Mahindi wilayani Mvomero Mzee Mohamed Kigonile akizungumza na watafiti wa mradi wa AGRISPARK shambani kwake Wami Dakawa.

“Tunajua nyinyi watafiti kutoka kwenye Chuo chetu kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) mnafanya kazi nzuri na tafiti nzuri kutusaidia wakulima tuzalishe kwa tija, sasa tusaidieni kama kuna tafiti mlizofanya kuhusu wadudu hawa mtuletee tujifunze ili zitusaidie kuwatokomeza maana kwa uwezo wetu sisi tumefika mwisho tunahitaji msaada wenu na serikali mtuokoe njaa itatumaliza” alieleza Mzee Kigonile.

Akizungumzia tatizo hilo Mtafiti mkuu mwenza wa mradi wa AGRISPARK kutoka SUA Dkt. Nicholaus Mwalukasa amewaambia kuwa amepokea maombi yao hivyo wanakwenda kutafuta machapisho ya kisayansi mbalimbali ambayo yamefanyika kuhusu namna ya kupambana na wadudu hao na wakiyapata wataandika vitabu vidogo ambayo vitaelezea na kufundisha namna ya kuwadhibiti wadudu hao.

“Tulipokuwa kwenye kata ya Nyandira pia wakulima wametoa kilio hichocho kwa wadudu hao katika zao la mahindi hivyo sisi kama watafiti tunalichukua na kwenda kulifanyia kazi maana tunamini zitakuwepo tafiti ambazo zimefanyika na kuchapishwa kwenye majarida ya kisayansi ya kimataifa ambayo sio rahisi nyinyi kuyafikia lakini sisi tutafanya hivyo kwa niaba yenu na kuwaletea kwa lugha rahisi ili muweze kuelewa” alifafanua Dkt. Mwalukasa.

 Watafiti hao wa mradi wa AGRISPARK kutoka SUA wametembelea wakulima kwenye wilaya ya Mvomero, Morogoro Manispaa na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Vijijini na kukutana na wakulima na kuungumza nao kuhusu mahitaji yao ya elimu kwenye shughuli za kilimo na changamoto zinazowakabili ili wweze kuwatafutia ufumbuzi wa changamoto zao kwa kuandaa vitabu vidogo vya kuwaelimisha kuhusu mahitaji yao.

Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya jamahuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.


Kiwavijeshi vamizi akiwa kwenye mmea wa mhindi shambani akishambulia mazao.



Post a Comment

0 Comments