SUAMEDIA

TPHPA yaahidi kufuatilia changamoto ya Nzi weupe Nyandira Wilayani Mvomero zilizotolewa na wakulima kupitia mradi AGRISPARK - SUA

Na: Calvin Gwabara – Mvomero.

Kufuatia taarifa za athari kubwa za Nzi Weupe kwenye mazao ya mbogambona Wilayani Mvomero zilizoibuliwa na wakulima wakati wa utekelezaji wa mradi wa AGRISPARK Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru ameahidi kutuma timu ya wataalamu kwenye wilaya hiyo kuona athari na kufanya oparesheni ya kuwatokomeza wadudu hao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru (Picha kwa msaada https://afrikaleo.co.tz/)

Mkurugenzi huyo mkuu wa TPHPA amesema amesikia taarifa zilizolipotiwa na vyombo vya habari kuhusu kilio cha wakulima wa Nyandira, Wilaya ya Mvomero, Mkonai Morogoro lakini hakuna taarifa rasmi iliyowasilishwa na Halmashauri kwenye ofisi yake kwaajili ya kuhitaji msaada kwenye kuwakabili wadudu hao ambao wanashambaulia mazao ya wakulima.

“Sisi tunafanya kazi nchi nzima katika kupambana na majanga ya wadudu mbalimbali na ndege ambao wanaathiri mazao ya wakulima lakini utaratibu unaotakiwa kufuatwa ni Maafisa ugani wa kata kupeleka taarifa kwenye ofisi za halmashauri, halafu halmashauri wakishajiridhisha wanatakiwa kutuandikia barua kuomba msaada wetu na sisi huwa tunachukua hatua mara moja maana hata hivi sasa wataalamu wetu wapo kwenye mikoa mbalimbali wakifanya kazi hizo kusaidia wakulima” Alisema Prof. Ndunguru.

Aliongea “Tunamshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya Kilimo kwa kuendelea kuiwezesha TPHPA kwa kutupatia zana za kisasa za kupambana na visumbufu vya mimea kwa kutupatia Madawa ya Ruzuku lakini pia vitendea kazi ikiwemo ndege zisizo na rubani (Drone) na ndege kubwa kwaajili ya kupulizia dawa kwenye mazao na  hii inatusaidia kuwafikia wakulima wengi zaidi tofauti na awali”.

Prof. Ndunguru amesema kuwa taasisi yake ipo kwaajili ya kuwahudumia wakulima pale wanapopatwa na majanga makubwa ya wadudu na magonjwa ambayo yanahitaji vifaa na uwezo mkubwa wa kupulizia madawa hivyo wanapopata changamoto hizo wasisite kufuata taratibu ili waweze kusaidiwa kwa haraka.

Amesema hivi karibuni wanatarajia kupokea ndege nyingine moja kubwa ya kisasa kwaajili ya kuongeza nguvu katika kupulizia dawa kwenye mazao kwa kuwa tayari imeshalipiwa na itawasili muda wowote kuanzia sasa ili kusaidia ndege moja kubwa waliyonayo hivyo wanatarajia itaongeza sana ufanisi katika kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea.

Kwa upande wake mtafiti Mkuu mweza wa mradi wa AGRISPARK –SUA Dkt. Nicholous Mwalukasa ambao vilio hivyo wa wakulima vilitolewa mbele yao na kuomba wawasaidie kupaza sauti zao kwa serikali amesema taarifa hiyo ya TPHPA wataifikisha kwa wakulima na maafisa Ugani kwenye kata hizo ili waweze kufuata taratibu zilizoanishwa na kuweze kusaidiwa.

Kwa upande wake mtafiti Mkuu mweza wa mradi wa AGRISPARK –SUA Dkt. Nicholous Mwalukasa akizungumza na wanafunzi wa mradi huo mara baada ya kuzungumza na wakulima kuhusu changamoto hiyo.

“ Tunamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TPHAPA Prof. Ndunguru kwa kuamua kuchukua harua za haraka kuwasaidia wakulima hao mara tu baada ya kumfikishia taarifa hizo na tunaamini wakulima hao wataweza kupata suluhisho changamoto hiyo ya wadudu na kulima kilimo chenya tija” alisema Dr. Mwalukasa.

Aliongeza “Kwa mujibu wa Prof. Ndunguru amesema zipo njia rahisi zaidi zinazoweza kutumiwa na wakulima katika kudhibiti wadudu hao hivyo sisi kama mradi tutafuatilia tuzipate na kisha kuandaa vitabu vidogo ambavyo wakulima watapewa na kuweza kupambana na wadudu hao”

Wakulima wa mbogamoga Kata ya Nyandira wilayani Mvomero waliibua na kuwasilisha changamoto hiyo ya wadudu kwa Watafiti wa mradi wa AGRISPARK waliokuwa kwenye wilaya hiyo kwa lengo la kuzungumza na wakulima kupata changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kutokana na machapisho mbalimbali ya kisayansi yaliyopo na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo waliobobea kwenye maeno hayo.

Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya jamahuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.


Muonekano wa Nzi weupe wakiwa kwenye mmea picha kwa hisani ya mtandao.



Post a Comment

0 Comments