SUAMEDIA

Nzi weupe wanavyoacha umasikini kwa wakulima wa mbogamboga Nyandira

 Na: Calvin Gwabara – Nyandira.

Wakulima wa Kata ya Nyandira Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wamewaomba watafiti wa Mradi wa AGRISPARK unaotekelezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kuwatafutia mbinu za kukabiliana na wadudu aina ya Nzi weupe (White flies) ambao wanaathiri mazao yao na kusababisha upotevu wa zaidi ya asilimia 70 hadi 80.

Picha hii kwa msaada wa :https://www.ugaoo.com/blogs 

Ombi hilo limetolewa na wakulima hao wakati wa Watafiti kutoka SUA waliokwenda kukutana na wakulima kutambua changamoto na mahitaji yao ya maarifa ambayo ili kuandaa machapisho kwa lugha ya Kiswahili ambayo yatawaongezea maarifa wakulima na hivyo kuwasaidia kuboresha kilimo chao na kuinua kipato cha kaya hizo zilizo kwenye eneo la mradi huo wa utafiti wa AGRISPARK.

Mkulima Peregrin Adam akizungumza na Wanafunzi watafiti wa mradi wa AGRISPARK kuhusu athari za Nzi weupe kwenye mazao yao.


Akizungumza na watafiti hao Mkulima Peregrin Adam kwa niaba ya wakulima wenzake amesema kuwa wadudu hao hivi sasa wamekuwa tishio kwa wakulima shambani na hakuna dawa ambayo kwa sasa inaweza kuwaangamiza kwakuwa wamekuwa wengi na unapojaribu kupuliza dawa wanaruka ikiisha wanarudi na kuendelea kushambulia mazao.

“Tumefurahi sana kuwaona watafiti kutoka SUA kuja kututembelea na kujua changamoto zinazotukabili, Kusema ukweli kwa sasa changamoto kubwa kwenye kata hii yote ni hawa wadudu weupe huku tunawaita “Masister” kutokana na weupe wao, hakuna dawa tena inayoweza kuwaua wadudu hawa na wamejaa mashambani wanashambulia zaidi zao la maharage ambalo ndilo zao letu kubwa la biashara kwenye kata yetu” Alieleza bwana Peegrini.

Aliongeza” Kiukweli kwa sasa kilimo kimekuwa kigumu sana maana wanashambulia karibu mazao yote ya mbogamboga ambayo ndio tegemeo letu kwa kipato kwa wakulima wote kwenye kata hii, na wanatupa hasara kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mazao yanapotea kutokana na mashambulizi yao”.

Nae Adam mkulima mwingine wa Nyandira ameiomba SUA kupitia kwa watafiti wake kuwasaidia kupata ufumbuzi wa tatizo hilo na ikiwezekana kufikisha kilio hicho kwa serikali na wizara ya Kilimo kuwatafutia ufumbuzi wa wadudu hao ambao wanawapa umasikini wakulima wengi kwa sasa.

“Mkiangalia kwa mazingira yetu huku tunalima mbogamboga msimu wote na tunategemewa sana kwa kuzalisha maharage hasa mabichi kwenda mikoa mbalimbali hasa Dar es salaam na Dodoma lakini kwa sasa uzalishaji wetu umepungua mno kutokana na kuongezeka kwa wadudu hawa hatari wasiosikia dawa” alisema bwana Adam.

    Kwa upande wake Mtafiti Mkuu mwenza wa mradi wa AGRISPARK Dkt. Nicholous  Mwalukasa amesema kuwa lengo la kuwatembelea wakulima hao ni kutaka kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo ili waweze kutumia uwepo wa machapisho mbalimbali ya kisayansi yaliyopo kuandaa vitabu vidogo ambavyo vitakuwa na mada mbalimbali  ili kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto zao ili kuongeza uzalishaji.

“ Hivi sasa tupo kwenye hatua ya tatu ya mradi ambapo tumekuja kupata maelezo na changamoto zenu ili twende kuwatafutia ufumbuzi wake kupitia tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani kote na kwa kutumia wataalamu wa SUA na taasisi zingine na baadae tutatayarisha kwa lugha rahisi ambayo mtaweza kuelewa na kutumia elimu hiyo kutatua changamoto hizi” Alieleza Dkt. Mwalukasa.

Aliongeza “Kwanza niwape pole kwa changamoto mnayokutana nayo kwa wadudu hawa na sisi tumelichukua na tunakwenda kuwatafutia majibu sahihi na ya namna ya kuwakabili wadudu hawa pamoja na changamoto zingine mlizoziainisha, tutaziandaa katika nakala ngumu na nakala laini na kuwaletea ili muweze kupata maarifa hivyo kuendelea kulima kilimo chenye tija na kujikwamua kujipatia maendeleo kupitia kilimo cha mbogamboga mnachokifanya zaidi katika eneo hili”. 

Watafiti hao kutoka SUA kupitia mradi wa AGRISPARK wapo kwenye zoezi la kutembelea kata zilizo ndani ya mradi huo kwenye Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini kwaajili ya kukutana na wakulima na wafugaji kutambua mahitaji yao ya maarifa yanayoweza kusaidia kuinua uzalishaji kupitia kilimo na mifugo katika mnyororo mzima wa thamni wa mazao na mifugo yao.

Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kama maono mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwaajili ya kuwawezesha watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WAKULIMA HAO WAKIZUNGUMZA NA WATAFITI KUHUSU CHANGAMOTO ZAO KWENYE KATA YA NYANDIRA.










Post a Comment

0 Comments