Na: Siwema Malibiche
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimeendelea kuhakikisha mafunzo kwa vitendo yanafanyika kwa ubora na ufanisi mkubwa ili kuzalisha wataalamu wabobezi
watakaoisaidia jamii kwa kutoa huduma bora itakayopelekea maendeleo kwa Taifa.
Hayo yamesemwa na Mhadhiri kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi ya Afya iliyopo SUA Dkt. Mungo Ngalameno alipozungumza na SUA Media wakati wa
mitihani ya vitendo inayoendelea kufanyika katika Kampasi ya Edward Moringe mkoani Morogoro
ikihusisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza
kutoka Shahada ya Awali ya Utabibu wa Wanyama ambapo amesema SUA inatengeneza
misingi bora kwa kuzalisha wataalamu wenye ufanisi na ubora kwa jamii.
Aidha Dkt. Ngalameno ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwa wanafunzi ikiwemo maabara na vifaa vyake na kusema Wahadhiri wanaendelea kuhakikisha wanafunzi kutoka chuoni hapo wanakuwa na ubora utakaosaidia kutibu wanyama na kuisaidia jamii inayowazunguka huku akijivunia kuwepo kwa wataalamu wengi wa tiba ya wanyama nchini katika Sekta mbalimbali waliozalishwa SUA.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Shahada ya Awali ya Utabibu wa Wanyama Bakiri Azizi amekiri kufurahishwa na kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo kwani anaamini yatamsaidia kutatua changamoto kwa urahisi na kuwataka wale wote wanaotamani kujiunga na masomo yao SUA waweze kujiunga ili wafaidike na elimu bora inayotolewa na Chuo hicho.
Naye Mwanafunzi wa Shahada ya Awali ya Utabibu wa Wanyama SUA Gradness Roman amesema anajivunia kuwa SUA na anatamani idadi ya wanafunzi wanawake iongezeke kwani bado kumekuwa na imani potofu kuwa wanawake hawawezi kusoma masomo ya udaktari wa wanyama.
Mafunzo kwa vitendo SUA hufanyika kwa ufanisi kutokana na kuwepo kwa miundombinu na uangalizi mkubwa wa walimu kulingana na masomo husika ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi na ubora unaotakiwa kwa maendeleo ya taifa.
0 Comments