Na: George Alexander
Wito umetolewa kwa wanafunzi
nchini wanaonufaika na ufadhili mbalimbali wa masomo kuzingatia na kuheshimu masomo
yao pamoja na ufadhili wanaoupata ili waweze kuhitimu masomo yao kwa wakati.
Wito huo umetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza na wanafunzi wanufaika wa ufadhili wa masomo wa mradi wa Climate Action Network Tanzania (CAN) kwenye warsha iliyofanyika SUA na kuwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Prof. Chibunda amewataka
wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu na pia kujiheshimu ili kuweza
kuthamini mchango walioupata kwa wafadhili wa masomo yao na kuwawezesha
kumaliza kwa muda uliopangwa.
“Niwapongeze sana utaratibu wa
ufadhili wa SAMIA Scholarship kwa utaratibu waliojiwekea kwa mwanafunzi
asipofikisha ufaulu wa GPA ya 3.8 ufadhili wake unasitishwa na kupewa mtu mwingine katika Chuo hicho hicho,
hii inapelekea mwanafunzi kusoma kwa bidii”, amesema Prof Chibunda.
Aidha Prof. Chibunda amewapongeza
CAN kwa kuwa wazalendo wa kutafuta pesa kwa wafadhili mbalimbali na kuamua
kuzileta nchini na kusaidia wanafunzi wa Kitanzania ambao asilimia kubwa hushindwa
kutimiza ndoto zao kwa kukosa mahitaji muhimu ya shule.
Dkt. Sixbert Mwanga ambaye ni Mtafiti na Mkurugenzi wa Shirika la CAN amevitaja vigezo mbalimbali vilivyotumika kuwapata wanufaika hao ikiwa ni pamoja na kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambayo imebainisha mikoa maskini, lakini pia wanafunzi ambao hawana ufadhili wa Serikali (BOOM) na kutumia fomu mbalimbali kwenda kwa wenyeviti wa vijiji na watendaji pamoja na kuhitaji wanafunzi ambao wanasoma masomo yenye tija vijijini mfano kilimo, ufugaji, utalii wa vijijini.
“Tumeingia mkataba na wanafunzi
na kila mwaka watakuwa wanajaza mkataba mpya na pia tutafuatilia maendeleo ya
mwanafunzi kwa kutumia matokeo yake lakini pia kufuatilia maendeleo yake
kupitia kwa wakuu wa idara na hii itatufanya tujue kama mwanafunzi ataendelea
na ufadhili au tumsitishie na tumpe mtu mwingine”, amesema Dkt Sixbert.
“Idadi ya wanafunzi 36 kati ya
300 walioomba wamepata nafasi kupitia tangazo tulilolitoa kwa mwezi mzima huku
wasichana wakiwa idadi kubwa na sio kwa upendeleo bali kwa vigezo walivyokidhi,
na sio Tanzania Bara tu hadi wanafunzi wa Tanzania Visiwani tumewachukua”, amesema
Dkt. Catherine
Mwanafunzi mmoja wapo ambaye ni
mnufaika wa ufadhili huo anayesoma Udaktari wa Mifugo mwaka wa nne Ampelius
Anthony amesema safari yake ya elimu mpaka kufikia hapo ilikuwa ni ya kusuasua kwani
alilazimika kuwahusisha viongozi wa Chuo
na wakati mwingine kuchangiwa karo.
“Binafsi niushukuru uongozi wa
SUA kwa kututangazia kila fursa inayokuja hususani inayohusu ufadhili wa masomo
nina ahidi kuwa na juhudi na kuweza kutimiza ndoto yangu ili niweze kusaidia
jamii”, ameeleza Ampelius
Mikoa ambayo wanafunzi wake
wataweza kunufaika na ufadhili wa masomo unaotolewa na CAN Tanzania ni Kagera,
Shinyanga, Singida, Lindi, Manyara, Mtwara, Mara, Morogoro, Unguja ambapo wanafunzi
watakaopata ufadhili huo ni wale wa kuanzia ngazi ya Cheti, Astashahada,
Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili.
0 Comments