Na: Farida Mkongwe
Watafiti wametakiwa
kushirikisha makundi mbalimbali ya jinsia zote katika hatua za awali za utafiti
wao ili kupata taarifa zitakazoisadia Serikali kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii pamoja na kupanga mipango ya
maendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugeni wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Devotha Mosha Januari 17, 2025 wakati akizungumza na SUA Media kwenye warsha ya kuwajengea uwezo watafiti wachanga katika ukusanyaji na uchakataji wa takwimu ili kupata tafiti zilizo bora zenye manufaa kwa jamii, taasisi na taifa kwa ujumla.
Dkt. Devotha ambaye pia ni
Kiongozi wa Kitengo cha Jamii katika masuala ya jinsia kwenye Mradi wa Utafiti wa Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) amesema
watafiti wanatakiwa kutumia mbinu shirikishi na kushirikisha makundi yote
wakiwemo wanawake, wanaume, wazee, vijana, matajiri, maskini na makundi mengine
ili kupata taarifa zitakazogusa makundi yote kwenye jamii.
“Kama mnavyojua bila mbinu shirikishi huwezi kupata
taarifa zilizo sahihi ambazo zinajitosheleza katika kutoa mapendekezo
mbalimbali katika taasisi zetu na kwa Serikali pia, hivyo nitumie fursa hii
kutoa wito kwa watafiti wanaposikia kuna mafunzo ya aina hii wajitahidi
kushiriki kwa wingi ili kuja kujifunza na kujiendeleza ikiwa ni pamoja na
kuzijua hizi mbinu shirikishi ambazo zina faida kwa jamii”, amesema Dkt.Devotha.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo akiwemo Egata Makanja kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Rehema Mollel Mkufunzi Msaidizi, Idara ya Maendeleo na Mafunzo ya Kimkakati kutoka SUA wameupongeza mradi wa CLARITY kwa kuandaa warsha hiyo ambayo imekuwa na faida kubwa kwao.
“Pale NDC tuna miradi mingi ya maendeleo hivyo mafunzo
haya yatanisaidia kufanya tafiti mbalimbali ili kupata taarifa zilizo bora
ambazo tutazichakata na kuzisambaza kwa jamii kwa matumizi mbalimbali”, amesema
Makanja.
“Nimefurahi sana kupata nafasi hii kwa sababu nilikuwa natamani kujifunza kwa muda mrefu, japokuwa tumejifunza darasani lakini haikuwa kwa uwanja mkubwa kama tulivyofundishwa hapa, naona kabisa mafunzo haya yameniongezea maarifa katika utendaji wa kazi zangu”, amesema Rehema.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamedhaniniwa na
Mradi wa CLARITY yamewakutanisha pamoja washiriki 70 na wengine zaidi ya 100 wameshiriki
kwa njia ya mtandao ambapo wote wamepewa vyeti vya ushiriki.
PICHA ZOTE NA AYOUB MWIGUME
https://drive.google.com/
0 Comments