SUAMEDIA

SUA yaendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia ili kuzalisha wakulima wenye tija

 

Na: Siwema Malibiche

 

Katika kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inakuwa kwa kasi zaidi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuboresha miuondombinu ya kujifunzia kwa wanafunzi wake kwa kuhakikisha wanafanya mafunzo kwa vitendo ya kutosha yatakayowawezesha kuwa wataalam wabobezi watakaochangia maendeleo kwa Chuo na Taifa kwa ujumla.


Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Mashamba ya Mafunzo kutoka SUA Bw. Roman Mfinanga wakati akizungumza na SUA Media kwenye zoezi la uvunaji wa matikiti na matango uliofanyika katika shamba la mafunzo SUA lililopo Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro ambao  ulihusisha wanafunzi wa mwaka wa pili huku akieleza namna ambavyo wanafunzi wameshiriki kuanzia kuandaa mashamba hayo mpaka kufikia hatua ya mavuno.



Aidha  Bw. Mfinanga ameishukuru Menejimenti ya Chuo kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Chuo hicho inayowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo kulingana na fani wanazosomea ikiwemo  kilimo cha mboga mboga na amewakaribisha wananchi wote kutembelea SUA kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu kilimo kwa maslahi ya Taifa.


Naye Afisa Kilimo wa Idara ya Mashamba ya Mafunzo kutoka SUA Bi.  Khalima Mrisho amesema utaratibu wa mafunzo kwa vitendo umeendelea kuboresha mazingira ya Chuo na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi thabiti ambao unatokana na jitihada za walimu wao kuwasimamia kikamilifu  na kuleta matokeo mazuri kwa jamii.

Kwa upande wao wanafunzi wa mwaka wa pili kutoka SUA  Elisha Poul  na Hadija Omary wakiwa ni miongoni  mwa wanafunzi walioshiriki katika uvunaji wa matikiti na matango wamesema kupitia shughuli mbalimbali zinafanywa na Chuo, Wanafunzi wanajifunza kwa vitendo kuanzia uandaaji wa shamba mpaka uvunaji lakini pia upatikanaji wa mbegu na namna bora ya usimamizi wa shamba jambo ambalo linawasaidia kupata ujuzi utakaotumika kama fursa ya kujiajiri  baada ya kumaliza Chuo.


Zoezi hilo la uvunaji wa matikiti na matango lililofanyika katika Shamba la Mafunzo SUA  limeendelea kuwawezesha wanafunzi kufanya kwa vitendo yale yote ambayo wanajifunza kwa nadharia kwa ushirikiano mkubwa wa wasimamizi wao ambapo wanafunzi hao hushirikishwa kuanzia hatua za mwanzo za uandaaji wa shamba hadi uvunaji.








Picha zote na Mabula Mussa




Post a Comment

0 Comments