SUAMEDIA

SUA yatoa mafunzo kwa watafiti wachanga ili kuzalisha tafiti bora

 

Na: Farida Mkongwe

Katika kuhakikisha tafiti zinazofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi nyingine zinakuwa na manufaa kwa jamii, Chuo hicho kupitia Mradi wa Utafiti wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) kimetoa mafunzo kwa watafiti wachanga wakiwemo wanafunzi wa SUA ya namna ya kukusanya na kuzichakata takwimu ili kuzalisha tafiti zenye ubora.



Akizungumza na SUA Media Januari 16, 2025 kuhusu mafunzo hayo ya siku mbili yanayofanyika SUA, Kiongozi Mkuu wa Mradi wa CLARITY Prof. Japhet Kashaigili ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti , Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam SUA amesema kuna umuhimu mkubwa kwa watafiti wachanga kujua mbinu za kukusanya takwimu kwa utaratibu unaofaa na kuzichakata ili kuwa na manufaa yanayotarajiwa.

“Ni kipindi ambacho watafiti na wanafunzi wetu wa SUA wapo katika kipindi cha ukusanyaji wa takwimu, sasa tukasema kabla hawajaanza au wakati wakiendelea kuchukua takwimu tuwajengee uwezo ili waweze kuzijua mbinu bora za kuchukua takwimu, mfano umekusanya takwimu sasa uanze kazi ya kuzichakata, unazichakataje, unachakata kwa kutumia mbinu gani, ili upate nini, kwa manufaa ya nani, kimsingi hayo ndiyo malengo yetu ndiyo maana mafunzo hayo yanatolewa kwa nadharia na  vitendo”, amesema Prof. Kashaigili.



Naye Prof. Kim Abel Kayunze kutoka Idara ya Taaluma za Maendeleo na Mafunzo Mkakati SUA ambaye ni miongoni mwa wawezeshaji katika mafunzo hayo amesema hayo ni mafunzo ya utafiti shirikishi na kuwahimiza washiriki wazingatie wanachofundishwa sambamba na kusoma vitabu na majarida ambayo yamenukuliwa wakati wa mafundisho hayo ili wapate utaalamu wa kina utakaowasaidia kufanya tafiti zitakazotatua changamoto za jamii.



Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo hayo Mbonea Joshua Mweta kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za Mazao ya Misitu SUA ambaye pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani wanahitaji kuwa watafiti nguli na hawawezi kuwa watafiti kama hawajui namna ya kukusanya takwimu na kuzichakata “nina imani mafunzo haya yatanisaidia kwa kiasi kikubwa”.




Mtafiti Msaidizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Bertha Manga ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Maendeleo Vijijini SUA amesema elimu anayopata kwenye mafunzo hayo ni muhimu sana kwa mustakabali wa masomo yake pamoja na kazi anayofanya kwani tayari yeye ni mtafiti.







 Picha zote na Ayoub Mwigune 

ZAIDI BOFYA LINK HAPO CHINI

https://drive.google.com/drive/folders/1fX5YgapKaqxxUZKgAyeqS931j-pT-NvX

Post a Comment

0 Comments