SUAMEDIA

Viongozi Serikali ya Wanafunzi na wawakilishi wa madarasa SUA wajengewa uwezo

 Na: Adamu Maruma

Baadhi ya viongozi wa Serikali ya Wanafunzi  (SUASO) na Wawakilishi wa wanafunzi  (CRs) kutoka Kampasi za Edward Moringe, Solomon Mahlangu, na Mizengo Pinda  wamejengewa uwezo kwenye maeneo mbalimbali katika  semina ya siku moja iliyoandaliwa na Dawati la Jinsia  SUA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi ,iliyofanyika  kwenye ukumbi wa  MLT 9  Kampasi ya Edward Moringe  Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo  SUA.

Makamu Mwenyekiti wa  Dawati la Jinsia SUA Dkt. Emma Njau aliyesimama kulia akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoibuliwa na washiriki

Akizungumza katika semina hiyo Makamu Mwenyekiti  wa Dawati la Jinsia SUA, Dkt. Emma Njau amesema semina hiyo ambayo pia imeshirikisha Dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi imelenga kuwajengea uwezo wanafunzi ambao ni viongozi  wa Serikali ya Wanafunzi  kwenye maeneo   ya muhimu ili wawe salama wawapo chuoni hapo.

‘’Leo hii tumekuwa na semina  ya kuwajengea uwezo wanafunzi ambao ni viongozi  tukilenga Serikali ya Wanafunzi na wawakilishi wa madarasa (CRs) ili kuwajengea uwezo kuhusu mambo ambayo  ni muhimu kwao wakiwa  hapa chuoni, kama vile mambo yanayohusu mitihani, masuala ya malazi, namna ya kutumia muda wao vizuri, magonjwa ya aina mbali mbali yakiwemo yanayotokana na ngono, na mada zilizohusu Dawati la Jinsia na tulipata mwakilishi kutoka Jeshi  la Polisi Morogoro aliyezungumzia kuhusu ukatili wa Kijinsia’’ , amesema Dkt. Njau.

Dkt. Njau ameongeza kuwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi hao viongozi  ni kuwawezesha  kutoa  elimu kwa wanafunzi wenzao wanaowaongoza  katika maeneo hayo makuu yaliyofundishwa na wanategemea wanafunzi hao kuwa msaada kwa wenzao hasa kwa kipindi hiki wanapojiandaa na mitihani yao.

Washiriki wa Semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi ambao ni Viongozi wa Serikali ya Wanafunzi na Wakilishi wa Madarasa wakiwa katika picha ya pamoja na  wawezeshaji wa semina hiyo.

Amewakaribisha wanafunzi  kufika katika dawati la Jinsia  SUA ili kujifunza kazi zinazofanywa na dawati hilo lakini pia wasisite kufikisha malalamiko yao yanayohusu ukatili wa kijinsia na  wamejipanga kuwahudumia kwa uaminifu  mkubwa ili kupambana na matukio ya kikatili pindi yanapoibuka chuoni hapo kwani lengo la dawati nikuhakikisha SUA inakuwa  sehemu salama kwa wanafunzi, pamoja wanajumuia wote katika eneo la ukatili wakijinsia.

Kwa upande wao  Felister Mwakapeje  Waziri  wa Jinsia na Mahitaji Maalum  SUA na  Reuben Jeremiah Mwakilishi  wa Wanafunzi  kozi  ya Uchumi Kilimo na  Biashara mwaka wa kwanza wamesema semina hiyo imewajenga vizuri katika maeneo yaliyoanishwa  na kuahidi kwenda kuwa mabalozi kwa kuwafikshia wanafunzi wenzao mambo waliyojifunza.

Katibu wa Kamati ya maandalizi ya semina Ndg. Kelvin Msawile kushoto akiteta jambo na mwakilishi wa wanafunzi wanaosoma shahada ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia muda mfupi kabla ya kuanza semina

Naye Dkt. Kiondo Solomon kutoka Hospitali ya SUA  amewashauri wanafunzi  kuishi kwa kujali afya zao kwa kujikinga na tabia hatarishi zitakazowasababisha kupata maradhi mbalimbali yakiwemo magonjwa ya zinaa hali itakayopeleka kuharibu maisha yao na hivyo kuwa hasara kwao, familia na Taifa kwa ujumla.

Semina  hiyo ya siku moja kwa viongozi wa Serikali ya Wanafunzi na Wawakilishi wa Madarasa imewashirikisha  wanafunzi wa  Kampasi ya Mizengo Pinda ambapo walishiriki kwa njia mtandao (Zoom Meeting) na waliweza  kuchangia mada  zilizowasilishwa  na  wawezeshaji wa  semina hiyo .





Post a Comment

0 Comments