Na: Winfrida Nicolaus
Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
imeipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi na kuboresha Mitaala ambayo imezingatia mahitaji, uhalisia lakini pia
kumkomboa mwananchi wa kawaida pamoja na kukabili changamoto zinazozuia watu
kufikia malengo yao ya kukidhi soko la ajira kidunia.
Amebainisha hayo Rais wa Serikali ya Wanafunzi SUA Bw. Hatibu Kilenga wakati akizungumza na SUA Media namna walivyoipokea na kuelewa uboreshwaji wa Sera hiyo ambapo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyoboreshwa imeonesha kuangalia zaidi mahitaji ya nchi kisekta ikiwemo maeneo yanayofaa kuongezewa mkazo kwa ajili ya kupata wataalamu kwa wingi zaidi ambapo kupitia hilo wameona namna wanavyoenda kunufaika kwenye Kilimo eneo ambalo limeonekana lina upungufu wa wataalamu karibu 66%.
Aidha amesema kuwa Sera hiyo imewekwa kwenye muktadha ambapo
inaonesha ujuzi utakaotolewa umeakisi kumjengea mtu maarifa ambayo anaweza
kuyatumia kwenye kuleta mabadiliko hivyo hiyo inampa mtu fursa ya kujifunza sio
tu kwa ajili ya kuajiriwa lakini pia kujiajiri mwenyewe.
“Kwenye eneo la Sayansi na Teknolojia ukisoma ukurasa wa 31
kwenye Sera hiyo Serikali inaenda kuweka mazingira ya upatikanaji wa kitabu
kimoja bora cha kujifunza na kumuwezesha mtu kuelewa ukilinganisha na hapo awali ambapo tulikuwa na vitabu vingi
kwa ajili ya mwanafunzi kuvipitia na kuelewa maudhui mazima kwa ajili tu ya
kujibu mitihani”, amesema Kilenga.
Kwa upande wake Felister Mwakapeja Waziri wa Jinsia na Watu wenye Mahitaji Maalumu katika Serikali ya Wanafunzi SUA amesema kupitia Sera hiyo ameona namna Serikali imeweza kuwa na mchango katika kuongeza rasilimali watu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na ubaguzi wa rangi, jinsia wala kubagua watu wenye mahitaji maalumu lengo likiwa kuhakikisha kila mtu anapata elimu ambayo ni haki yake ya msingi.
Vile vile wameweza kuona jitihada za Serikakali katika
kuongeza viwango vyenye ubora zaidi katika elimu na mafunzo ambapo jitihada
hizo zimeweza kufanikiwa kupitia kutengeneza mazingira rafiki na salama ya
kujifunza kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu lakini pia kutengeneza
mitaala yenye tija na ufanisi na yenye kukidhi mahitaji na vigezo vya soko la
ajira.
Naye Makame Ally Waziri wa Katiba, Sheria, Bunge na Utawala
Bora Serikali ya Wanafunzi SUA amesema katika Sera hiyo Serikali imekuja na
mpango wa elimu huria ambayo itamuwezesha mtu kusoma huku akiendelea kufanya
majukumu yake mengine kwa kuwa atajifunza kwa njia ya mtandao hivyo kupunguza
msongamano wa kufundisha wanafunzi wengi katika eneo moja.
“Lakini pia hii inaonesha ni namna gani Tanzania tunaweza na
tunaendelea kupambana na kuikimbiza Teknolojia kutoka kwenye ufundishaji wa
maandishi ya ubaoni kwenda kujifunza kwa njia ya mtandao ambapo pia
imewarahisishia waajiri ambao wangepunguza nguvu kazi kwa ajili ya mtu kwenda
masomoni lakini sasa atasoma huku akiwa eneo lake la kazi”, amesema Ally.
Sera Mpya ya Elimu ya Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na
Mitaala iliyoboreshwa itazinduliwa rasmi
na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Januari 31, 2025 jijini Dodoma.
0 Comments