Na: Siwema Malibiche
Idara ya Sayansi ya Wanyama, Ukuzaji wa Viumbe Maji na Nyanda za Malisho ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeendelea kujidhatiti katika kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na jamii, ikiwa ni juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo nchini.
Mkuu wa Idara na Naibu Rasi wa Ndaki ya Kilimo Prof. Antony Sangeda akizungumza na SUA Media |
Akizungumza na SUA Media, Mkuu wa Idara hiyo na Naibu Rasi wa Ndaki ya Kilimo, Prof. Antony Sangeda, amesema idara hiyo ni moja ya idara kongwe, ikiwa na historia ya miaka 55 kufikia mwaka 2024 tangu kuanzishwa kwake huku ikiwa tayari imeongozwa na zaidi ya wakuu wa idara 13 na kwa sasa inahudumia zaidi ya wanafunzi 1,800.
Prof. Sangeda ameongeza kuwa Idara ina miundombinu ya
kisasa ikiwemo mashamba ya mafunzo yanayosaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo
na maabara zinazotumika kupima ubora wa vyakula vya mifugo, bidhaa za wanyama
kama maziwa na nyama, pamoja na usindikaji wa maziwa yanayozingatia afya na
ubora kwa mlaji.
Aidha, mashamba hayo hutumika kwa mafunzo ya ufugaji wa Kuku, Sungura, na Nguruwe, wanyama hao hutumika kwa tafiti, mafunzo kwa vitendo na kuelimisha jamii, ambapo wataalamu wa SUA wanashirikiana na wakulima ili kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu bora za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitengo cha Mifugo cha Idara hiyo, Dkt. Khaji Mkata, ameipongeza menejimenti ya SUA kwa kuwekeza katika Idara hiyo na kueleza kuwa wamefanikiwa kuwafikia wananchi kwa kiasi kikubwa, amesema juhudi zaidi zinahitajika ili kuboresha huduma na mafunzo wanayotoa.
Naye, Meneja wa Kitengo cha Ufugaji wa Viumbe Maji, Bw. Charles Makondo, amesema kitengo hicho kimejikita katika ufugaji wa samaki aina ya Sato, Kambare, na samaki wa mapambo.
Pia, wanazalisha mimea kama Azola na magugu maji kwa ajili ya chakula cha Samaki, kitengo hicho pia kinatoa huduma za ugani, mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na jamii, pamoja na uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya kambare kwa ajili ya wakulima.
Kuangalia makala fupi bofya kiunganishi hapa chini 👇
https://youtu.be/NBHepbpTeVY?si=aLy2-_WaG9JerdJJ
0 Comments