SUAMEDIA

Hongera SUA kwa kuinua taaluma na kilimo nchini - Mhe. Pinda

 Na: Mwandishi wetu.

Waziri Mkuu Mstaafu wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Mizengo Pinda ameipongeza Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuhakikisha wanainua taaluma na kilimo nchini.

Mhe. Pinda aliyesimama katikati akisikiliza maelezo kutoka kwa Naibu Rasi wa Ndaki ya Mizengo Pinda Prof. Makindala wa pili kutoka kulia

Mhe. Pinda ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake katika Ndaki ya Kampasi ya Mizengo Pinda ambayo ni moja ya Ndaki za SUA, Mkoani Katavi kwa lengo la kujionea shughuli za maendeleo chuoni hapo.

Amesema ana imani kubwa na SUA kwani hata ujenzi wa majengo mapya unaofanywa katika Kampasi hiyo utachochea ongezeko kubwa la wanafunzi na Shahada mbalimbali zitakazochochea mabadiliko ya kiuchumi katika eneo  hilo, mkoa na mikoa ya jirani.

Aidha, Mhe. Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya za kuinua  elimu na uchumi kwa wananchi katika mkoa  wa Katavi, kupitia Mradi  wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ambao utachochea maendeleo ya Chuo, mkoa na wananchi kwa Ujumla.



Katika ziara hiyo Mhe. Pinda amepata fursa ya kuzungumza na watumishi pamoja na wanafunzi  kisha kwenda kujionea maendeleo ya mradi unaofanywa na kampuni ya Til Construction.

SUA imeendelea kuboresha miundombinu yake kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi HEET,  ambapo Kampasi ya Mizengo Pinda iliyopo mkoani Katavi imetengewa kiasi cha fedha Dola za Kimarekani Milioni nane.






Post a Comment

0 Comments