SUAMEDIA

Wakulima nchini pimeni udongo - Dkt. Boniphace Massawe

 Na: Siwema  Malibiche,

Wakulima  nchini wametakiwa kupima udongo kabla  ya kuanza shughuli za kilimo  ili kujua zao na mbolea inayofaa kabla ya kulima ili kuepusha hasara inayoweza kutokea.

Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia SUA  Dkt. Boniphace Massawe  akizungumza wa waandishi wa habari 

Hayo  yamebainishwa Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Udongo na Jiolojia SUA  Dkt. Boniphace Massawe  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika siku ya maonyesho ya  kilimo  ya Chuo  yaliofanyika  katika Chuo Kikuu cha  Sokoine cha Kilimo   Kampasi ya Edward Moringe  Mkoani  Morogoro ambapo amewataka wakulima kuacha kilimo cha mazoea  badala yake wanatakiwa kujikita zaidi  kwenye kuzingatia afya ya udongo ili kupata faida.

Aidha, amesema kuwa  kama taasisi imeleta maonyesho hayo kwa wakulima na wadau wake ili kuongeza uelewa juu ya afya ya udongo kwa kutumia tafiti mbalimbali zinazofanyika ili kuwawezesha wakulima  kupata maendeleo walioyatarajia  huku akiongeza kuwa  afya ya udongo ikiimarishwa nchini  itasaidia  kukuza sekta ya kilimo.

Wanafunzi waliofikia kujionea na kujifunza namna ya kupima udongo wakipita katika mabanda ya maonesho

Kwa upande wake,  Mratibu wa Utafiti wa Udongo  Tanzania kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano cha Mkoani Tanga Dkt. Sibaway Mwango  amesema ni jukumu la kila mkulima kuhakikisha ubora wa afya ya udongo  kwa kuzingatia kuwa  kila udongo una mbolea zake ambazo zikitumika vyema zinaweza kumpatia mkulima tija na pale mkulima anapokosea na kuweka mbolea isiyofaa kwenye udongo fulani hupelekea kupunguza tija na hata kupata hasara kabisa.

Amesema, wamefika SUA ili kuonyesha teknolojia mbalimbali kwa jamii  zitakazowezesha kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo ili kuwa na kilimo cha kisasa na cha kibiashara  na kuleta mendeleo kwa mkulima na taifa kwa ujumla huku akikiri uwepo wa wakulima wengi ambao hawana uelewa  juu ya afya ya udongo.

Nae, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Wanaagromia Tanzania Bw. Emmanuel Zephaline kutoka TAS  ambao ndio waandaaji wa maonyesho hayo amesema  kama taasisi  hiyo   itaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya utunzaji  na upimaji wa udongo ili kukuza sekta ya kilimo nchini kwa  kuzalisha chakula chenye ubora na kutosha

Maonyesho hayo  yanafanyika SUA  kuelekea  siku ya udongo duniani ambayo  ina adhimishwa  disemba 05   kila mwaka, maonyesho hayo  yanahusisha wadau mbalimbali wa kilimo wakiwemo TARI, Taasisi ya Wanaagromia Tanzania  (TAS ), SUA na kampuni binafsi zinazojishughulisha na sekta ya kilimo

Picha chini ni matukio mbalimbali katika maonesho hayo 👇







Post a Comment

0 Comments