Na: Farida Mkongwe
Baadhi
ya wakulima wa zabibu na wajasiriamali wanaotengeneza mvinyo jijini Dodoma
wamekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) chini ya Mradi wa Elimu
ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa kuandaa mafunzo ya vitendo juu ya
utengenezaji mvinyo bora ambayo wanakiri yataongeza thamani katika Mvinyo
wanaotengeneza.
Wakizungumza na SUA Media Desemba 4, 2024 mara baada ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutengeneza mvinyo bora katika Kiwanda cha Utengenezaji Mvinyo cha Alko Vintage (Dodoma) wakulima hao akiwemo Bw. William Swai kutoka Hombolo, Bw. Steven Barie kutoka Mradi wa Zabibu na BBT Chinangali, Bi. Gloria Shayo kutoka Mvumi na Bw. Innocent Njau kutoka Mkonze wamesema mafunzo hayo yamewaongezea utambuzi wa namna ya kuandaa mvinyo mzuri wenye ubora wa kimataifa.
“Nafurahi
na kuishukuru SUA kwa sababu mafunzo ya mwezi June, 2024 yalitupa ufahamu tu wa
jumla, lakini leo hapa kiwandani tumeona mashine na vifaa mbalimbali
vinavyotumika kusindika mvinyo, hii inatuhamasisha kufikia hatua hizi”, amesema
Bw. Swai ambaye anaomba Serikali iwasaidie kurahisisha upatikanaji wa vifaa
bora vya kutengeneza mvinyo bora.
“Kupitia mafunzo haya naamini nitawasaidia watu wa Chinangali hasa kwenye mradi wa zabibu tutashirikiana na wataalamu wenzangu katika kuhakikisha tunazalisha zabibu iliyo bora na kutengeneza mvinyo katika kiwango chenye ubora wa juu ambacho tumejifunza kupitia SUA”, amesema Bw. Barie.
Bi. Gloria amewataka wanawake kuingia kwenye sekta ya viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji mvinyo kwa kuwa ni biashara nzuri na yenye faida “mimi najivunia SUA na nawashukuru sana kwani awali nilikuwa sijui vitu vingi lakini kwa sasa hata wateja wameongezeka maana nimejifunza misingi muhimu ya uzalishaji zabibu likiwemo suala la usafi.
Naye
Bw. Njau ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha Pilot Wine amesema kabla ya kupata mafunzo
kutoka SUA alikuwa amejikita kufanya utafiti wa kupata masoko ya mvinyo “lakini
baada ya kupata mafunzo haya nikapata elimu ya kuweza kutengeneza mvinyo na
siyo mvinyo tu bali mvinyo bora na salama”.
Mtengenezaji
mvinyo kutoka Kampuni ya Alko Vintages Bw. Archard Kato akitoa mafunzo hayo kiwandani
hapo amesema nia yao ni kuboresha mvinyo unaotengenezwa Dodoma ili kulinda nembo
ya mvinyo jijini humo, akisema “tumesisitiza misingi ya utengenezaji mvinyo
ulio bora na lengo ni kuwafaanya wazalishaji wadogo waelewe umuhimu wa kuwekeza
kwenye misingi hiyo, tunajitahidi sana kushiriki kutoa mafunzo kwa sababu
inatusaidia kueneza elimu tuliyo nayo,”.
Mtafiti Mwandamizi kutoka TARI MAKUTUPORA Bi. Felista Mpore amesema wameandaa mafunzo hayo ili kuwapa wakulima wa zabibu na watengenezaji wa mvinyo uelewa mmoja wa njia sahihi za usindikaji wa mvinyo kuanzia uchaguzi wa zabibu shambani hadi kwenye kufungasha mvinyo “ tukisema mvinyo wetu huu wa Dodoma uwe na mfanano iwe mvinyo mweupe au mwekundu, watumiaji watakapoonja tu wasema huu mvinyo umetoka Dodoma”.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Kilimo kutoka Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) SUA Bw. Philipo James amesema mafunzo hayo ni kutimiza moja ya lengo la SUA kupitia Kitengo cha Ugani katika kuhakikisha wanawafikia wakulima na kuwapa elimu bora ya kilimo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Awamu
hii ya pili ya mafunzo imewawezesha wazalishaji hao wa mvinyo kupata mafunzo
kwa vitendo ambapo katika awamu ya kwanza walipata mafunzo ya nadharia, mafunzo
yote hayo yanafanyika chini ya Mradi wa HEET kwa kushirikiana na Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo (TARI - MAKUTUPORA).
0 Comments