Na: Adam Maruma
Vijana wasomi wa vyuo vikuu wametakiwa kueleza mambo
mazuri yaliyopo barani Afrika kupitia uandishi wa vitabu kwani ndio njia
inayoweza kuwakomboa watu wengi kifikra na kuondokana dhana ya utegemezi bila
ya misaada kutoka mataifa ya nje.
Katibu wa Jumuia ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania, (TAHLISO) Akilimali Mwasampinde akizindua kitabu anayefuatia kulia kwake ni mwandishi wa kitabu hicho Bw. Gasper Mwita |
Hayo yamesemwa na Katibu wa Jumuia ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu Tanzania, (TAHLISO) Akilimali Mwasampinde alipokuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa
Kitabu kilichoandikwa na mwanafunzi wa
Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Gasper Mwita
Francis chenye anuani ya Fikra Huru za Mwafrika ambacho kinaelezea umuhimu
waafrika kujikomboa kifrika katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na
kijamii.
Mwasampinde amesema bara la Afrika lina mambo mengi
mazuri na hakuna mtu ambaye atatoka
nje ya bara hilo kueleza mambo hayo na ni muda sasa wa vijana
waliobahatika kufikia ngazi ya elimu ya juu kutumia maarifa waliyopata vyuoni,
kuwaelimisha wenzao fursa zilizopo barani humo na kuzitumia ili kujikwamua kiuchumi na kifikra.
''Ukiangalia bara hili lina mambo
mengi mazuri kuliko mambo ambayo yanaelezwa na mataifa ya magharibi kama vile,
vita, njaa, ukame na mengine hivyo ni wakati wa vijana haswa wasomi wa vyuo
vikuu kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zilizopo na kuzitumia kujikwamua kiuchumi
na kifikra na hakuna atakayetoka nje ya bara hili na kuja kueleza mambo hayo''
amesema Mwasampinde.
Aidha amempongeza mwandishi wa kitabu hicho chenye
jina la ''FIKRA HURU ZA MWAFRIKA'' ndugu Gasper Mwita Francis kwa kuweza
kuandika kitabu hicho ambacho amesema kinakwenda kufungua mawazo ya watu kujiamini na kujiamulia mambo yao kwa
mustakabali wao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mwandishi wa kitabu hicho Gasper
Mwita Francis amesema ameandika kitabu hicho ili kuchochea mtazamo huru wa
kifikra na kimapinduzi kwa vijana wa
bara la Afrika, hususani Tanzania na
hilo litawezekana endapo watasoma kitabu hicho na kuyafanyia kazi yaliyoandikwa
ndani yake.
Ameongeza kuwa fikra huru ni silaha muhimu kwa vijana
kuweza kufuata nyayo za wazalendo wataifa hili kama muasisi wa taifa, Hayati Mwl.
Julius Nyerere na Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Hayati Edward Moringe
Sokoine ambao walipenda kuona Taifa linasonga mbele kiuchumi hali iliyowafanya
kutumia muda wao mwingi kusoma vitabu
vilivyowaongezea ufahamu wa namna ya kuliongoza
taifa katika imani ya kazi kama msingi wa maendeleo.
Amewasihi vijana kujenga utamaduni wa kujisomea
vitabu vyenye maarifa mbalimbali ili kuweza kuongeza ufahamu wa mambo
mseto hali itakayo wajengea kujiamini na
kuchambua mambo kwa kina hivyo kufanya maamuzi sahihi kwa masilahi yao na
taifa kwa ujumla.
Mwandishi Gasper Francis Mwita ni mwandishi chipukizi
ambae kitabu chake cha Fikra Huru za
Mwafrika ni muendelezo wa kazi yake
uandishi wa vitabu kwani amendika vitabu katika nyanja zingine ikiwemo dini, na
vitabu vya hamasa ili kuchochea ukuaji wa maendeleo, amani na utulivu nchini.
0 Comments