Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimezindua mradi wa tathmini ya mapato ya kaboni kama njia endelevu ya uwezeshaji kifedha katika uhifadhi na usimamizi wa misitu ya jamii Tanzania. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Rafiki Hotel, Mkoani Dodoma na kuwatanisha wadau mbalimbali wa misitu kutoka takribani mikoa tisa ya Tanzania Bara.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Profesa Maulid Mwatawala akizungumza katika uzinduzi huo |
Aidha
Prof Mwatawala ameongezea kusema kuwa SUA kama mdau mkubwa wa mazingira
itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi kwa kuwawezesha kupata
elimu bora ya utunzaji wa mazingira na kupelekea wananchi kunufaika kupitia
misitu. Sambamba na hilo amewashukuru watafiti kutoka SUA ambao ni Dr. Kajenje,
Dr. Mbeyale na Dr. Lyimo kwakuja na mradi ambao utasaidia uhifadhi endelevu wa
misitu na biounuai.
Pia
amewashukuru wafadhili wa mradi ambao ni Idara ya
Mazingira Chakula na Masuala ya Vijijini ya Uingereza (Department for Environment, Food and
Rural Affairs (Defra) of
United Kingdom) kwa
ushirikiano na Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Serikali ya Uingereza na
Shirika la maendeleo mbadala (Development Alternatives, Inc. (DAI). Na pia amekishukuru Chuo Kikuu cha
Bangor cha nchini Uingereza kwa kukubali kushirikiana na watafiti wa SUA
kutekeleza mradi huu. Aidha ametoa shukrani
za pekee kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia
Suluhu Hassan kwa kuwa msitari wa mbele kuunga juhudi za Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo katika uhifadhi kwa manufaa
ya nchi.
Awali Daktari Kajenje
Magessa Nkukurah ambaye ni Mhadhiri wa SUA na mtafiti kiongozi wa mradi
alibainisha kuwa lengo la mradi ni kuangalia namna gani wananchi wanaoishi
katika maeneo yanayozungukwa na misitu wanaweza kuhifadhi misitu wenyewe bila
kuiathiri na kuepusha mabadiliko ya tabia nchi, kutunza bioanuai na kuboresha
hali yao ya kimaisha .
Pia alieleza kuwa pato
la bionuai halijafanyiwa utafiti katika
nchi yetu lakini linaweza likachangia kwa kiasi kikubwa uhifadhi endelevu
katika maeneo ya misitu yenye bioanuai ya kipekee.
Aidha
amebainisha kuwa mradi huo utakuwa wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 mpaka
2027, huku akiainisha mikoa takribani mitano itakayonufaika na mradi huo
ikiwemo mikoa ya Manyara, Katavi, Tanga, Kilimanjaro pamoja na mkoa wa Morogoro
ambayo ipo Tao la mashariki yenye misitu yenye bioanuai ya kipekee. Na kuongezea
kuwa katika mikoa miwili ya Manyara na Katavi tayari wamekwisha anza biashara
hiyo ya kaboni hivyo pia watatumika kama wawezeshaji kwenye mikoa mitatu ambayo
wana nia kuanza kufanya biashara hiyo.
Pamoja na hayo Dkt
Kajenje aalisema kuwa jamii zitakwenda kunufaika moja kwa moja na mradi huu kwa
kujengewa uwezo wa namna gani wataweza kunufaika na biashara ya kaboni.
Naye
Afisa misitu mkuu Felister Magembe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) amebainisha kuwa ofisi yake inafanya kazi kwa karibu na
wananchi. Hivyo itashirikiana na Chuo cha SUA katika kuwawezesha wananchi
kupata elimu juu ya utunzaji endelevu wa misitu ili kufanya mikoa hiyo iweze
kunufaika. Amesema kuwa baadhi ya
vijiji ambako kuna miradi ya kaboni vimenufaika na kuweza kujenga shule, vituo
vya afya na barabara kwa kupitia biashara hiyo.
Kwa
upande wake Sanura Mshana ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mazingira kata ya
Shinghatin Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni mmoja wa washiriki katika Warsha hiyo
amesema kuwa mradi huu umekuja wakati muafaka kwakuwa baadhi ya maeneo wananchi
wamekuwa wakiharibu mazingira na kuingiza mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Hivyo mradi huo utachangia kuleta suluhu katika uhifadhi wa misitu iliyo maeneo
yenye bioanuai ya kipaumbele Tanzania (Biodiversity hotspots)
0 Comments