SUAMEDIA

Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Mashariki yahitimisha wiki ya Maadili kwa kishindo.

 Na: Adam Maruma.

Sekretarieti ya Maadili ya Umma Kanda ya Mashariki imehitimisha maadhimisho ya wiki ya maadili na haki za binadamu katika Kampasi ya Edward Moringe, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro ambapo shughuli mbalimbali vya kijamii  zimefanyika na tume hiyo kwa kushirikiana na Taasisi zingine za serikali na binafsi mkoani humo.

 Kiongozi wa Tume ya Maadili Kanda ya Mashariki Hendry Sawe akichangia damu katika Wiki ya Maadhimisho ya Maadili na Haki za Binadamu

Miongoni  mwa   shughuli  zilizogusa maisha ya watu kwa kiasi kikubwa ni cha uhamasishaji wa uchangiaji  damu ambapo Maafisa wa Tume ya Maadili  wakiongozwa na Katibu Msaidizi na Mkuu wa Kanda ya Mashariki Bw. Henry Sawe wamechangia damu pamoja na wananafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Cha Morogoro na Chuo Kikuu Mzumbe ambapo shughuli hiyo ilifanyika katika vyuo vyote viwili kwa lengo la kusaidia watu wenye uhitaji wa damu.

Mbali na hayo, Tume pia imehamisha zoezi la upandaji miti   ya matunda 100 katika kata ya Magadu ambapo shughuli hiyo imeongozwa na Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala ambapo ameipongeza Tume kwa kuendelea na shughuli ya utoaji elimu ya

Baadhi ya wafanyakazi wa SUA walioshiriki maadhimisho hayo kwa kupanda miti Hospitali ya Sabasaba Morogoro Mjini

maaadili na utunzaji wa mazingira ili kuunga jitihada ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha mazingira.

''Pamoja na kwamba serikali ipo katika mkakati wa kuanza kufundisha elimu ya Maadili kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi vyuo vikuu niwapongeze tume ya Maadili kanda ya mashiriki kwa kuendelea kutoa elimu ya Maadili pamoja na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wetu wa Morogoro'', amesema Mh. Kilakala

Kwa upande wake kiongozi wa Tume ya Maadili Kanda ya Mashariki Hendry Sawe amewataka viongozi katika taasisi mbalimbali kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji wa majukumu yao na  amewataka wananchi kutoa taarifa wanapoona uvunjifu wa sheria na maadili huku akiwataka kushiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo kujitolea na kutunza miundombinu iliyowekwa na Serikali kwa maendeleo ya taifa.

Naye, Afisa kutoka Idara ya Damu Salama Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro, Bw. Kwilasa Kakila amesema kuwa wapo kuhakikisha zoezi la kuchangia damu linaenda sawa na kuongeza kuwa tendo la kuchangia damu kwa jamii linasaidia kuokoa maisha ya watanzania wenye uhitaji kama vile wamama wajawazito ,watu waliopata ajali na wagonjwa wa  Selimundu .

Pia, amewatoa hofu wanaosita kuchangia damu kuwa zoezi hilo halina madhara na ni salama ili kuokoa maisha ya watu huku ikizingatiwa kuwa mkoa wa Morogoro unatumia zaidi ya uniti 350 za damu kwa mwezi kwa wagonjwa mbalimbali na kuongeza kuwa kuna uhitaji mkubwa na amesisitiza kuwa jamii isisubiri hadi kuhamasishwa kutoa damu .

Kwa upande wake, Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA anayeshughulikia Utawala, Fedha na Mipango, Prof. Amandus Muhairwa  ambae alikuwa  mgeni rasmi siku ya kilele cha maadhimisho hayo ameupongeza  uongozi wa Sekretalieti ya Maadili Kanda ya Mashariki  kwa kuadhimisha siku ya maadali na kufanya shughuli za kijamii ambapo pia amewataka washiriki wote kuwajibika  na kuwa wazalendo kwa taifa huku akisisitiza kuwa maadili ni  chanzo cha kufanikiwa katika sekta zote

Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA anayeshughulikia Utawala, Fedha na Mipango, Prof. Amandus Muhairwa (kulia) akitoa zawadi kwa washiriki wa bonanza

Siku  ya maadhimisho ya siku ya Maadili  na Haki za Binadamu Kanda ya Mashariki imehitimishwa kwa kufanya bonanza la mchezo wa mpira wa miguu ambapo vyuo vikuu na vyuo vya kati   mkoani Morogoro vimeshiriki ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA , Chuo Kikuu Cha Waislamu Morogoro na Chuo cha Uwalimu wa Ufundi Stadi VETA ambapo pia elimu juu ya Maadili  na kupiga vita vitendo vya rushwa imetolewa kwa washiriki wa bonanza hilo.

Picha chini ni matukio mbalimbali katika maadhimisho hayo 






Post a Comment

0 Comments