SUAMEDIA

Kijiji cha Lubungo-Mvomero kuwa mfano wa Kilimo cha Mazao ya Bustani kibiashara

 

Na: Tatyana Celestine

Wananchi wa Kijiji cha Lubungo Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro hususani kinamama na vijana wamepata fursa ya kutatua changamoto ya masoko na teknolojia katika kilimo cha mazao ya bustani kibiashara kupitia Washirika wa Wahitimu wajasiliamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA (SUGECO) ambayo itatengeneza ajira zaidi ya 1820.

                                

Akizungumza katika Ufunguzi wa Mradi wa Vijana wa Kilimo cha Mazao ya Bustani  kibiashara Nov 7, 2024  Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameipongeza SUA kupitia SUGECO kwa kuonesha nia ya kuleta maendeleo katika kijiji hicho ikiwa ni ndoto yao ya miaka 12 iliyopita na kuamua kuifanya iwe kweli kwa kuanza kutekeleza mradi huo ambao utakuwa wa faida kwa wakazi wa wilaya hiyo pamoja na taifa kwa ujumla.

                         

Mkuu wa Mkoa huyo ametoa maagizo kwamba mradi huo ukawe faida kwa pande zote wananchi , Mkoa na hata Taifa kwa kufanya eneo hilo liwe mfano wa kilimo cha mazao ya bustani, kutatua ugomvi wa wakulima na wafugaji,  kutoa elimu katika maeneo jirani kujifunza kupitia SUGECO, pamoja na kulima kwa tija ili kubadilisha hali ya maisha yao kupitia kilimo hicho.

Aidha ametoa maagizo kupitia mradi huo heka 100 zitengwe kwa ajili ya malisho ya wafugaji ili  wasilishie mifugo katika eneo linalotekelezwa na mradi na nyingine 200 zigawiwe kwa wakulima katika kijiji hicho ili nao waweze kujifunza kilimo kutoka kwa wataalamu wa SUGECO kwa kufanya hivyo migogoro ya wakulima na wafugaji ibadilike kuwa fursa kwa kutegemeana wakulima walime na wafugaji wazalishe Samadi kwa ajili ya kilimo .

                                        

Mhe. Malima ameagiza Benki ya CRDB kuhakikisha wakulima watakaoanzisha mashamba katika maeneo hayo wanawapa mikopo kwa vikundi ili waweze kufanya kilimo chao kuwa na tija bila kuhofia uwekezaji wao ambao baada ya kuuza mazao yao waweze kurejesha mkopo na wengine wapate ili kuendelea kukuza kilimo bustani nchini.

Akimwakilisha Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda,  Mkuu wa Idara ya Uchumi Kilimo na Biashara Dkt. Fulgence Mishili amesema Chuo kimekuwa bega kwa bega na SUGECO kwa utafiti pamoja na utaalamu lakini pia kimetoa eneo kwa ajili yao ni kwasababu wanaamini wanafanya kazi nzuri tangu kuanzishwa kwao 2021.


Naye Mkurugenzi wa SUGECO Bw. Revocatis Kimario amesema kuwa mradi huo ni mpango wa kutekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha vijana wanaweza kujiajiri kupitia kilimo unaoratibiwa na Wizara ya Kilimo chini ya programu ya BBT mazao mkakati ni pamoja na vitunguu, Matango, SweetMelon, Bamia, Nyanya chungu na Kerella (Britter guard).

                         

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa mradi huo utagharimu zaidi ya kiasi cha shilingi Bilioni 1.13  ambapo Programu ya Beyond Frming Collective (BFC) utachangia zaidi ya Milioni 926 na SUGECO itachangia zaidi ya shilingi milioni shilingi 208 ambapo fedha hizo zitatumika kupanua juhudi za SUGECO kuwekeza kwenye kilimo kupitia Kizimba Business Model katika kuweka miundombinu ya umwagiliaji, Teknolojia mpya na vifaa vya kisasa katika shughuli za kilimo ikiwemo matumizi ya nishati ya jua na mfumo wa umwagiliaji.

                        

Walipotakiwa kuzungumzia kwa namna gani wameupokea mradi katika eneo lao wananchi ambao ni wakulima na wafugaji katika eneo hilo wamesema ujio wa mradi huo utachangia kuinua kilimo cha mazao ya bustani kibiashara na hata wao kufaidika kwa kupata soko la uhakika lakini elimu watakayoipata kutoka SUA itawasaidia kuweza kulima kilimo cha tija kwani mradi huo umekuja mahususi katika kutekeleza mpango wa Youth Initiative For Agribusiness (BBT) ikiwa ni juhudi za serikali kwa vijana kujiajiri.


Mradi huo umedhaminiwa na Program ya Beyond Farming Collective (BFC) kwa ufadhili wa Bills and Melinda Gates Foundation umelenga kupanua mfumo wa kizimba Bussiness world Model (KBM) ambao unatekelezwa na Washirika wa Wahitimu wajasiliamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA (SUGECO).

                               

 
                                
                                    











                                







Post a Comment

0 Comments