Na: Calvin Gwabara - Dodoma.
Wataalamu wa Sayansi za Mimea
Vipando nchini wamekutana jijini Dodoma kujadili nafasi yao katika kusaidia kukabiliana
na visumbufu vya mimea vinavyochagiwa na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza
uzalishaji na afya ya mlaji.
Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kisayansi wa chama cha Wataalamu wa Sayansi za mimea vipando Tanzania (CROSAT). |
Akiongea kwenye mkutano huo Rais
wa Chama cha Wanataaluma wa Sayansi za Mimea Vipando Tanzania (CROSAT) Prof.
Kalunde Sibuga ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) amesema mkutano huo wa mwaka umeanza kwa mafanikio makubwa kwa kupokea
mada na mawasilisho mbalimbali ya mimea vipando kupitia tafiti zinazofanyika
ndani na nje ya nchi.
“Tumepokea na kujadiliana mada mbalimbali zinazohusu mimea
vipando, viuatilifu, visumbufu vya mimea na mbinu za kupambana na visumbufu
hivyo kwa njia ambazo hazitegemei tu madawa ya viwandani, lakini pia
tumejadiliana masuala mbalimbali ya kilimo ikolojia na faida zinazotokana na
kilimo hicho ikiwemo kuhifadhi bioanuai na mazingira kwa kuhakikisha
tunazalisha chakula ambacho ni safi na salama”, alieleza Prof. Sibuga.
Prof. Sibuga amesema Chama hicho
kinasaidia kutoa mawazo na michango chanya kwa Serikali na maendeleo ya kilimo
nchini kwa kutoa mapendekezo kuhusu masuala mbalimbali ambayo yanaathiri
uzalishaji na sekta ya kilimo kwa ujumla sambamba na kupokea maoni kwa wadau
wengine wa kilimo ili kutatua changamoto zinazowakabili kwa kutumia sayansi.
Kwa upande Mkurugenzi wa Idara ya
Uhauwilishaji wa Teknaolojia na Mahusiano kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania (TARI) Dkt. Sophia Kashenge amesema mkutano huo ni muhimu sana kwa kuwa
unawakutanisha wadau kuanzia Wakulima, Wanasayansi, watunga Sera na wadau wengine muhimu na kwamba ndani ya mkutano
huo kuna mawasilisho muhimu ambayo yanalenga kutatua changamoto za uzalishaji.
“Unaweza kuona mchanganyiko
mkubwa wa washiriki wa mkutano huu unasaidia sana kwenye kubadilishana mawazo
ya namna ya kutatua changamoto za kilimo kwa pamoja katika mazao mbalimbali,
lakini pia unasaidia kuwajengea uwezo na kuwaimarisha wanasayansi wachanga
katika taaluma hiyo ya sayansi ya mazao na sisi kama TARI tunajivunia sana
mkutano huu na umetoa fursa kwa watafiti wetu kueleza wanayofanya na changamoto
zake kupatiwa ufumbuzi”, alisema Dkt.
Kashenge.
Naye Nuhu Aman kutoka Taasisi ya
Utafiti wa Kahawa nchini amesema wao kama wanasayansi wachanga wanapata nafasi
ya kuvuna ujuzi kutoka kwa wanasayansi wakongwe lakini pia kupata ujuzi wa
namna ya kuandika na kuwasilisha matokeo ya tafiti za kisayansi kwa jamii na
wadau wengine.
“Hii ni fursa muhimu sana kwetu
kama wanasayansi wachanga kwenye taaluma hii kukutana na watafiti nguli ambao
wanasaidia kuboresha kazi zetu lakini pia kutuunganisha kati ya taasisi moja na
nyingine, kwa kweli tunajivunia kuwa
ndani ya CROSAT maana tunahudumiwa kufikia ndoto zetu” , alisema Nuhu.
Mkutano wa mwaka huu wa kisayansi
umebeba kauli mbiu isemayo “Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia
Teknolojia za Uzalishaji wa Mazao” na umewakutanisha wadau kutoka ndani na nje
ya Tanzania.
Mkurugenzi wa Idara ya Uhauwilishaji wa teknaolojia na mahusiano kutoka Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania TARI Dkt. Sophia Kashenge akizungumza kwenye mkutano huo.
Dkt. Yasinta Nzogela kutoka SUA akiwasilisha wasilisho lake kwenye mkutano huo. |
Dkt. Ramdhani Majubwa kutoka SUA akifanya wasilisho la utafiti walioufanya kuhusu kilimo Ikolojia. |
Prof. Eliningaya Kweka mwenyekiti wa kamati ya maandalizi kutoka TPHPA akizungumza kwenye mkutano huo. |
Dr. Wilson Nene kutoka TARI akitoa neno kwenye mkutano huo |
0 Comments