SUAMEDIA

Wanafunzi SUA watakiwa kuzingatia mafunzo kwa vitendo ili kuwa na uhakika wa ajira

 

Na: Siwema Malibiche

Wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kuzingatia mafunzo kwa vitendo yanayotolewa na Chuo hicho  kwa kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kukuza ufanisi wa kiutendaji na kuendana na soko la ajira lililopo nchini.




Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo Idara ya Mimea Vipando na Bustani SUA Bw. Wensislaus Milinga wakati akizungumza na SUAMEDIA  kwenye Kampasi ya Edward Moringe Sokoine Mkoani Morogoro alipokuwa akisimamia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa  Shahada ya Awali ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao  wakati wa mafunzo ya kuandaa shamba la mbogamboga.

Bw. Milinga amesema mafunzo kwa vitendo yanayotolewa chuoni hapo yana malengo mazuri na makubwa katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta ya kilimo.

Aidha, ameongeza kuwa SUA imeleta mafunzo kwa vitendo mapema kwa wanafunzi wapya wa  mwaka wa kwanza  ili kujua uwezo  na uelewa wao juu ya kilimo huku akibainisha kuwa kuna mwitikio mkubwa kwa wanafunzi hao kushiriki katika mafunzo ambapo inawasaidia kutunza kumbukumbu kwa kuhusianisha kile wanachokifanya shambani na watakachokisoma darasani.

Kwa upande wake Mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Shahada ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao Bw. Nais Isaya amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa kuandaa mazingira mazuri ya kuwawezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo ikiwemo mashamba ya kujifundishia wanafunzi yanayowasadia kuwajengea uwezo katika uzalishaji kwa kutumia teknolojia mbalimbali kuanzia  shambani  hadi sokoni.




Nao wanafunzi wa Mwaka wa kwanza wa Shahada hiyo ya Uzalishaji na Usimamizi wa Mazao Bi. Elizabeth Salimu  na  Bi. Elvira Rwechungura  wamewataka wanafunzi wote  kushiriki ipasavyo katika mafunzo kwa vitendo huku wakieleza  kuwa kilimo kinaweza kufanyika na mtu yeyote bila kujali jinsia



.Wameongeza kuwa wanawake wanatakiwa kujikita zaidi katika kuhudhuria na kushiriki katika mafunzo kwa vitendo  na  kutokata tamaa  kwa kutambua  kuwa fursa zinazopatikana kwenye kilimo zinaweza kumnufaisha mtu yeyote awe mwanamke au mwanaume.




Post a Comment

0 Comments