SUAMEDIA

Mkutano wa mwaka 2024 umebeba dhima ya Kukuza Ubunifu wa Kidigitali katika Kilimo Biashara Afrika.

Matumizi ya teknolojia katika kilimo yametajwa kuwa na mchango chanya katika kukuza na kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wakulima.

Hayo yamejiri wakati wa mkutano cha 16 cha kisayansi cha Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania (AGREST), uliofanyika Morogoro wakati wakijadili matokeo ya tafiti mbalimbali ya zilizofanywa na wanataaluma hao huku wakijikita katika kilimo digitali ambacho kinampa nafasi mkulima kutumia teknolojia kuongeza tija.

Mwenyekiti wa AGREST, Dkt. Florens Turuka amesema kama ambavyo teknolojia inatumika katika nyanja nyingine kama biashara, ni wakati wa sekta ya kilimo kuboreshwa kwa matumizi ya kidigitali ikiwemo katika kutumia akili mnemba, roboti na ndege isiyokuwa na rubani (drone ili kubaini changamoto za mazao shambani, kubaini aina ya udongo na mbolea gani itumike.

"Saizi mkulima hatakiwi kubahatisha kuhusu mbolea ya kutumia na hata kuuza mazao yake anaweza akasalia nyumbani akapata bei kwa njia ya kidigitali suala ambalo linampunguzia usumbufu na kufanya shughuli za kilimo kuwa rahisi tofauti na ilivyokuwa awali", alisema Dkt. Turuka.

Amesema kupitia kikao hicho, wanakusudia watatoka na mapendekezo mbalimbali ya kuishauri serikali ili ikione yanafaa waweze kuyaingiza kwenye sera zake.

Awali akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Bi. Isabela Maganga ameeleza kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo nafuu kwa ajili ya wakulima hasa kwa makundi maalumu, ambapo pia amesisitiza matumizi ya digitali katika uchumi kilimo ili kuendana na maendeleo ya teknolojia. 

Amesema kama ambavyo mtu anaweza kuagiza bidhaa au chakula sehemu na kuletewa alipo, hata kwenye kilimo inatakiwa tuanze kuona maisha kama haya, unaagiza nyanya kutoka shambani zinamfikia moja kwa moja mnunuzi au muhitaji.

Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania wamekuwa na utaratibu wa kukutana kila mwaka tangia kuanzishwa kwake lengo ni kuona kilimo kinakua sawa na maendeleo ya teknolojia kupitia mapendekezo mbalimbali ambayo mkutano huo huyatoa kwa serikali.









Post a Comment

0 Comments