Na,
Winfrida Nicolaus
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Kitengo cha Uhaulishaji wa
Teknolojia kwa kushirikiana na Youth Ignite Student Founders Fellowship
(StartHub Africa) kimefanya mafunzo ya kujenga mawazo ya bunifu kwa wanafunzi
chuoni hapo, ikiwa ni chachu ya kukuza ajira kwa kupitia biashara binafsi.
Amebainisha
hayo Afisa Msimamizi wa Uhaulishaji wa Teknolojia Bi. Lucy Madala wakati
akizungumza na SUAMEDIA baada ya mafunzo hayo ambapo amesema kupitia mafunzo
hayo wanafunzi wanasaidiwa kuweza kuja na dhana zinazoweza kutekelezwa katika
hali halisi za ulimwengu kibiashara hasa kwa kuelewa mahitaji na changamoto zinazoizunguka
jamii.
Bi. Lucy
amesema mafunzo hayo yamelenga kutatua matatizo au changamoto mahususi kupitia
vipindi vya kujadiliana, kuhimiza kufikiri zaidi na kujenga mazingira yanayofaa
kwa uzalishaji wa Mawazo kwa ushirikiano katika kuendeleza teknolojia, biashara
na uvumbuzi kwenye jamii.
Kwa
upande wake Bi. Shakila Mshana Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa StartHub Africa amesema Youth Ignite ni programu
ambayo imejikita katika kuwawezesha wanafunzi wa vyuoni ambao wana bunifu au
biashara zenye uwezo wa kufanikiwa kuingia sokoni na kuwawezesha kujiajiri wao
wenyewe lakini pia kutengeneza ajira kwa vijana wengine ili kujikwamua
kiuchumi.
Amesema
walianza kwa kuchagua vyuo kwa ajili ya kuendesha program hiyo na baadaye
katika kila chuo ikiwemo SUA wakafanya zoezi la usajili na kuchagua wanafunzi,
makundi au bunifu 30 kwa ajili ya kushiriki na kuwa sehemu ya program yao.
Bi.
Shakila amesema kwenye kila chuo wanaendesha kitu ambacho wanakiita kujenga
wazo thabiti kwa lengo la kuboresha
bunifu au biashara ambazo wanafunzi wanakuwa nazo ili wakiwa wanaenda
kwenye mchakato mwingine zinakuwa na ubora hivyo wanatoa mafunzo kwa kufundisha
mada mbalimbali ikiwemo ufanyaji wa tafiti kuhusiana na masoko, wateja vile vile
kuhakikisha wanaangalia tatizo vizuri kisha kuja na suluhisho kutoka kwenye
biashara au bunifu walizo nazo zenye kukidhi matakwa ya mlaji kuliko kitu
chochote.
“Baada ya
kutoa mafunzo na kuangalia endapo bunifu au biashara zao ziko sawa kwa maana ya
kuwaingizia fedha na je, zina faida na kama kuna changamoto wataweza
kukabiliana nazo kwa kujua nini cha kufanya na baada ya hapo tutaenda kwenye
hatua nyingine ya kushindanisha hizo biashara au bunifu kutoka kwa wanafunzi tuliowachagua kutoka katika
kila chuo na baadaye tutabaki na tatu bora kutoka kwenye kila chuo na
kushindanisha bunifu zao na watakaoshinda tutawashika mkono hatua kwa hatua ili
waweze kuendelea mbele”, amesema Shakila Mshana.
Naye Fanius
Merchades Mwanafunzi wa mwaka wa tatu, Shahada ya
Sayansi ya Chakula SUA ambaye ni mmoja wa washiriki kwenye program ya Start
Hub Afrika amesema amefurahi bunifu yake kuchaguliwa na kupata fursa ya
kujifunza kitu gani afanye ili kuboresha wazo lake kwa lengo la kufikia malengo
yake zaidi kukidhi matakwa ya soko la ajira ambapo kwa pamoja anaamini zoezi
hilo litawafanya wapige hatua zaidi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla lakini
pia kukiwakilisha chuo.
0 Comments