Wakati taifa likitarajiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba 2024, wananchi wa mtaa wa Mazimbu Kampasi wametakiwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa chama hicho kimekuwa uzoefu wa kutosha wa kuliongoza Taifa kwa miongo kadhaa sasa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya
ya Morogoro Mjini Komredi Abubakar Mdeng'o
wakati akizindua kampeni ya chama hicho na kumnadi mgombea wa Mtaa wa
Mazimbu Kampasi kwa tiketi ya chama hicho
Alex Bahame Alphonce katika
viwanja vya Freedom Square vilivyopo kampasi ya Solomon Mahlangu, Chuo Kikuu
Cha Sokoine cha Kilimo, SUA.
Komredi Abubakar Mdeng'o ambae
alikua mgeni rasmi katika ufunguzi wa kampeni za uchaguzi wa viongozi wa
serikali za mitaa mtaa wa Mazimbu Kampasi amewataka wananchi kuendelea
kukipatia chama hicho ushindi wa
kishindo kwa kuwa CCM imendelea kutekeleza ilani yake kwa ueledi mkubwa na
kuongeza kuwa hakuna sababu ya wakaazi
wa Kampasi hiyo kutowapa ushindi
viongozi hao kwakuwa wameonyesha utayari
wa kuwatumika katika kipindi cha miaka 5 ijayo.
Kiongozi huyo wa Vijana wa
CCM Morogoro mjini, amewataka viongozi
na wanachama wengine kushuka chini kwa wananchi kwa ajili ya kuwanadi viongozi
waliochaguliwa na chama ili viongozi hao waweze kupata ridhaa ya wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo
kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. John Nchimbi.
Kwa upande wake mgombea wa
Mtaa Mazimbu Kampasi Alex Bahame Alphonce amesema pindi wananchi watakapompa ridhaa ya
kuwatumikia yeye na wajumbe wake watahakikisha katika kipindi cha miezi miwili
ya mwanzo wa uongozi wake, Mtendaji wa mtaa huo, anapata ofisi ili wananchi
wapate huduma karibu na maeneo wanayoishi
ambapo kwa sasa wanachi hao wanalazimika kwenda umbali mrefu hadi kata ya Mindu kwa ajili ya
kupata huduma ya mtendaji huyo kwa kuwa Afisa huyo wa serikali ya mtaa wa
Mazimbu Kampasi hana ofisi katika mtaa huo.
''Mheshimiwa nimshukuru Rais
wetu kwa kutuletea afisa mtendaji katika mtaa wetu wa Mazimbu Kampasi,ila
kutokana na kukosekana kwa ofisi mtumishi huyu, anafanyia kazi zake kata ya
Mindu,sasa wananchi watakaponipa ridhaa hii ya kuwatumikia ndani ya miezi 2 ya
mwanzo, nitahakikisha kuwa Mazimbu
Kampasi kunakuwa na ofisi ya mtendaji wa serikali ya mtaa ili kumsaidia
mwananchi kuokoa muda na gharama ''
amesema Alex bahame.
Mgombea huyo ameongeza kuwa,
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza bayana kazi za
viongozi wa Serikali za Mitaa na yeye tayari anafahamu kazi iliyopo mbele yake
hivyo kuwataka wakaazi wa Mazimbu Kampasi kumpatia nafasi hiyo ili aweze kuwafanyia mambo
makubwa ambayo yamekuwa kero ya muda mrefu kama suala la uwizi,mifugo kuingia
ndani ya Kampasi hiyo na kuharibu mazao.
''Ndugu zangu mimepitia katiba
yetu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo kifungu cha 145 inazungumzia
Serikali za Mitaa na Kifungu cha 146
ukiisoma vizuri majukumu ni mengi
ila sisi kazi yetu ni kwenda kusukuma gurudumo la maendeleo mbele kutoka ngazi
cha chini kwenda juu '' amesema mgombea huyo
Katika hatua nyingine Mwakilishi wa Mkuu wa Ndaki ya Sayansi Asilia
na Tumizi Dkt. Beda John Mwang'onde alisema kuna Mambo mengi ya kujivunia kama mchango wa CCM katika
kampasi hiyo na kuwasihi wananchi kuupa
uzito uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuwa ni watu muhimu katika
kuwahudumia kwenye shughuli zao za kila siku .
Dkt. Mwang'onde ameongeza kuwa Kampasi ya
Mazimbu ina historia ndefu kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi imerithi baadhi ya
majengo ya Kampasi hiyo kutoka kwa
wapiginia uhuru wa Afrika ya Kusini , na
wamekuwa wakipokea wageni kutoka katika Taifa hilo la kusini mwa Afrika ambao
huja kujionea namna ndugu zao walivyoishi
katika eneo hilo.
Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa
Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake. Mojawapo ya madhumuni ya kuwepo kwa
serikali za mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi, na mwaka huu uchaguzi huo
unatarajiwa kufanyika mnamo Nov 27 2024 huku uchaguzi huo ukinadiwa kwa kauli
mbiu ya''𝘚𝘦𝘳𝘪𝘬𝘢𝘭𝘪 𝘻𝘢 𝘔𝘪𝘵𝘢𝘢 𝘚𝘢𝘶𝘵𝘪 𝘺𝘢 𝘞𝘢𝘯𝘢𝘯𝘤𝘩𝘪,𝘑𝘪𝘵𝘰𝘬𝘦𝘻𝘦 𝘬𝘶𝘴𝘩𝘪𝘳𝘪𝘬𝘪 𝘜𝘤𝘩𝘢𝘨𝘶𝘻𝘪 ''
0 Comments