SUAMEDIA

Wanafunzi wapya SUA wahimizwa kuzingatia masomo

 Wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliojiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wamehimizwa kuzingatia masomo wakati wote watakaokuwepo chuoni ili waweze kutimiza malengo ya kitaaluma.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mafunzo ya Awali kwa wanafunzi (Orientation Cource) SUA, Bi. Lydia Simion Bupilili wakati akitoa mafunzo kwa wanafunzi hao ambayo yanaendelea Kampasi ya Edward Moringe na Kampasi ya Solomon Mahlangu pamoja na kurushwa mbashara kwenye mtandao wa Youtube ambapo amesema imekuwa kawaida wanafunzi kushindwa kufikia ndoto zao za kimasomo kutokana na makundi rika.

Bi. Bupilili amewaeleza wanafunzi wanatakiwa kufahamu kuwa kila mmoja amefika SUA akiwa pekee yake na atarudi pekee yake, akiwataka kuepuka makundi rika ambayo hupelekea kuingia kwenye vitendo viovu ambavyo hushusha uwezo na ufanisi wa kitaaluma.

"Niwasihi wanangu, nimekuwa na uzoefu mkubwa kuhusu madhara ya kujiunga na makundi mabaya, kama hutakuwa na vipaumbele vya kufanya vizuri kitaaluma utajikuta unajiunga kwenye makundi mabaya ambayo yatashusha taaluma na kushindwa kufikia ndoto zako na mategemeo ya wazazi kwako", alisema.

Ameongeza kwa kuwasihi wanafunzi hao kuanza mapema kufikiria kuhusu maisha ya baada ya masomo ili waanze kufikiria kuhusu kuwekeza na uwekezaji kupitia elimu wanayopata, akisema kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa dhana ya ukosefu wa ajira.

Awali, Kaimu Mshauri wa Wanafunzi Bi. Hilda Gamuya akiwaelekeza umuhimu wa Ofisi hiyo kwa wanafunzi amesema muda wowote itakuwa wazi kutoa ushauri na kuwaelekeza wanafunzi kuhusu masuala ya kitaaluma, kiuchumi na kijamii ili wafikie ndoto zao za kimaisha.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinaendelea na mapokezi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao wanaendelea kuripoti pamoja na kuwapatia mafunzo ya awali ili kuwatengenezea mazingira rafiki kabla ya kuanza kwa masomo.





Post a Comment

0 Comments