Na:George Alexander
Halmashauri ya Mji ya Mbulu
Mkoani Manyara imewashukuru wataalam na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kwa kuwahamasisha wanafunzi wao kupenda na kusoma masomo ya
Sayansi ambapo imeonekana masomo hayo kukimbiwa na wanafunzi wengi.
Hayo yameelezwa na Afisa Elimu
Taaluma wa Halmashauri hiyo Bi. Elionora Nkata mara baada ya kupokea ugeni wa
wataalam wanne kutoka SUA kwa lengo la
kuhamasisha wanafunzi hususani wa kike kupenda na kusoma masomo ya sayansi
ambayo yameonekana ni tatizo kwa wanafunzi wengi.
Bi. Nkata ameeleza kuwa asilimia
kubwa ya wanafunzi ukata tamaa kwenye michepuo yao wanayosoma hususani ule wa
masomo ya kemia, bailojia na jiografia wakiamini kuwa mchepuo huo hauna masomo
ya kusoma chuo kikuu zaidi ya ualimu hivyo kupelekea wanafunzi wengi kufanya
chini ya kiwango na hata wengine kubadili mchepuo na wengine kuchagua masomo ya
sanaa wafikapo chuoni.
“Wanafunzi wengi wamekuwa
wakikata tamaa hususani wanaochukua mchepuo wa CBG maana wamekuwa wakiamini
hakuna kozi nyingine wakifika chuo watakayosoma kupitia mchepuo huo tofauti na
Ualimu, binafsi nawashukuru sana SUA kwa kuja sababu wanafunzi wametiwa moyo”
amesema Afisa Elimu huyo.
Ameongeza kuwa katika wilaya yake
jumla ya shule 15 kati ya 21 zinafundisha somo la kilimo hivyo imekuwa faida
kubwa kwa wilaya na kwa wanafunzi kwa sababu wanafunzi wamepata kuelekezwa kozi
mbalimbali zinazotolewa SUA na ufaulu ambao unatakiwa hivyo itachochea
wanafunzi wengi kusoma kwa bidii.
Aidha kwa upande wao walimu
wameonekana kufurahishwa na kuvutiwa na kile kinachofanywa na SUA kwa kuwatumia
wataalam wake ambao ni mabinti wadogo waliopata mafanikio kuja kuzungumza na
wanafunzi wao ambao wanakutana na vikwazo vingi vya kuzuia ndoto zao, ikiwemo
mimba na wengine kukatisha masomo yao kwa kuona wanapoteza muda.
“Wanafunzi wa ukanda huu wengi wana uwezo sana
wa masomo ya Sayansi na wengi huwa wanafaulu, lakini huwa tunashangaa wafikapo
kidato cha tano na sita baadhi uwezo wao hupungua na wengine wafikapo vyuoni huchagua
kozi za masomo ya sanaa” amesema mwalimu Shija Chile ambaye ni mwalimu wa somo
la baiolojia katika shule ya Chief Salwat.
Kwa upande wao wanafunzi wamewashukuru
sana SUA kwa kuwakumbuka na kufika katika shule zao huku wakieleza kutibiwa
majeraha yaliyokuwa yakiwasumbua kichwani mwao ya kuweza kusoma masomo ya
Sayansi lakini kutokana na kutokuwa na uelewa huamua kusoma masomo mengine
tofauti na masomo ya sayansi.
Lucia Faustine ambaye ni mwanafunzi
wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Tlaw iliyopo wilayani humo amesema
ameshawishika sana kuona wataalam na wahadhiri wenye umri mdogo ambao wamepata
mafanikio yao kupitia masomo na kutokupoteza muda na hata wengine kuwa na
taaluma mbili kama Daktari na Mhandisi.
Mwanafunzi huyo ameahidi atajitahidi
ili aje afikie malengo yake ya kusoma masomo ya sayansi na kubainisha kuwa
kupitia wataalamu hao amejua masomo ya Sayansi yana fursa nyingi za ajira
nchini.
SUA kupitia Mradi wa Elimu ya Juu
kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani HEET inaendesha programu maalum ijulikanayo kama
STEMI yaani Science, Technology, Engineering, Mathematics and Innovation kwa
awamu ya Pili katika Mkoa wa Manyara na Singida huku lengo likiwa ni kuwafanya
wanafunzi wengi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi.
0 Comments