Na: Farida Mkongwe
Baadhi ya wanafunzi waliohitimu masomo yao katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameahidi kuitumia elimu bora waliyoipata kwa vitendo katika kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, kuwasaidia wakulima pamoja na kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Wahitimu hao akiwemo Rahabu Kigali aliyetunukiwa Shahada ya Sayansi ya Lishe na Jamii, Janeth Nehemiah Shahada ya Uzalishaji wa Wanyama na Kayungilo Joseph Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Nyanda za Malisho wametoa kauli hiyo wakati wa Mahafali ya 44 ya Chuo hicho yaliyofanyika mjini Morogoro kwenye Kampasi ya Edward Moringe.
“Namshukuru Mungu kwa sababu nimejifunza mambo mengi katika kozi yangu na nina imani hii kozi itanisaidia sana kutoa elimu kwa jamii maana kwa sasa magonjwa bado ni mengi ambayo mengine yanatokana na kutozingatia suala la lishe, kwa hiyo mimi kama muhitimu katika masuala ya lishe nitashirikiana na wataalam kupunguza hili wimbi la magonjwa yanayotokana na lishe, tunajua ndiyo vyakula vipo lakini watu hawajui namna ya kuvitumia “, amesema Rahabu Kigali.
“Nitaisaidia jamii kuielimsha kwenye mifugo, watu wengi wanapenda kuwa wafugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe na mifugo mingine lakini hawana elimu ya kutosha ya ufugaji hivyo mimi nitatumia ujuzi na maarifa niliyoyapata SUA kuwasaidia wakulima, pia nawashauri vijana wajitokeze kwa wingi kusomea hizi kozi zinazohusu wanyama ni nzuri na zina manufaa makubwa “, amesema Janeth Nehemiah
Kwa upande wake muhitimu Kayungilo Joseph amesema SUA imemfundisha kujitegemea yaani kutokutegemea ajira ya Serikali badala yake kutumia fursa zinazopatikana katika jamii kujiajiri mwenyewe sanjari na kuisadia jamii upande wa wafugaji katika suala la malisho na kuwafanya wanyama kuwa na afya nzuri.
0 Comments