Na: Farida Mkongwe
Jumla ya wanafunzi 3061
wamehitimu masomo yao katika ngazi ya Shahada, Stashahada na Astashahada katika
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) huku idadi ya wanawake ikiendelea
kufanya vizuri kwa wanafunzi 1411 sawa na asilimia 46.1 ya wahitimu wote na
wanaume ni 1650 sawa na asilimia 53.9.
Akitoa takwimu hizo Oktoba 17, 2024 katika Mahafali ya 44 ya Chuo hicho Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema wahitimu wa Shahada za Awali wapo 2,809 ambapo kati yao wanaume 1,509 na wanawake ni 1,300, Shahada za Umahiri wahitimu 62 ambapo wanaume ni 34 na wanawake 28, Stashahada ya Juu ya Elimu wahitimu 3 wanaume wakiwa 2 na mwanamke 1, na wahitimu wa Shahada ya Uzamivu 25 kati yao wanaume 15 na wanawake 10.
Prof. Chibunda amesema wapo
wahitimu 120 wa Stashahada ambapo wanaume wapo 60 na wanawake 60 na wahitimu 42 wa Astashahada wanaume wakiwa 30 na wanawake 12 ambapo amewapongeza
wahitimu hao na hasa wanawake kwa kufikia hatua hiyo .
“Kwa hakika tunastahili
kujipongeza kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi
ya nguvukazi yenye taaluma, ujuzi na weledi ambao ni chachu ya kuongeza
maendeleo katika nchi yetu, aidha kwa kuzingatia kwamba kuhitimu SUA haijawahi
kuwa lelemama, kwa hiyo kwa dhati kabisa ya moyo wangu ninayo furaha kuwapongeza
wahitimu wote”, amesema Prof. Chibunda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Baraza la Chuo Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman amesema Baraza hilo
limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuboresha
mafunzo kwa vitendo na kuongeza ujuzi wa wahitimu.
“Baraza limeendelea kuhimiza
Menejimenti ya Chuo katika kutilia mkazo zaidi mafunzo kwa vitendo, kuboresha Mashamba
darasa, Karakana za Uhandisi, Maabara na Misitu ya Mafunzo ili kutoa fursa kwa
wanafunzi na wadau wengine wa kilimo kujifunza kwa vitendo ili kuongeza
maarifa, ujuzi na umahiri kwa lengo la kuboresha elimu, maarifa, ujuzi na kuwajengea wanafunzi umahiri wa stadi za maisha”, amesema Mhe. Chande.
0 Comments