Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimedahili jumla ya wanafunzi wapya wa Shahada za Awali 5,663
ambao wamesajiliwa na kuthibitishwa kujiunga na Chuo hicho hadi kufikia tarehe
11 Oktoba, 2024 katika mwaka wa masomo 2024/2025 huku mchakato wa kuthibishwa
kwa wanafunzi waliodahiliwa kwenye zaidi ya Chuo kimoja ukiendelea.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akizungumza kwenye Mahafali ya 44 yaliyofanyika mjini Morogoro kwenye Kampasi ya Edward Moringe Oktoba 17, 2024, ambapo wanafunzi 3061 wamehitimu masomo yao katika ngazi za Shahada, Stashahada na Astashahada.
Akielezea
majukumu yaliyotekelezwa na Chuo tangu
Mahafali ya 43 yaliyofanyika tarehe 23 Mei, 2024, , Prof.
Chibunda amesema SUA imeendelea kuboresha mitaala
yake ili kuendelea kutoa mafunzo yanayolenga kumjengea mwanafunzi ujuzi, weledi
na stadi za kujiajiri na kuajirika ikiwemo kuongeza fursa za kujenga ubunifu
kwa wanafunzi na kukuza stadi za kazi zinazozingatia viwango vya kimataifa.
“Jumla ya mitaala 99 (62 ya Shahada za Uzamili na 37 ya Shahada za Awali) ya Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo imefanyiwa mapitio na uhakiki na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, aidha mitaala 81 imewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu kwa ajili ya kuidhinishwa”, amesema Prof. Chibunda.
Ameyataja mafanikio mengine
kuwa ni Chuo kupata miradi mipya ya
utafiti 11 Katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 hadi Oktoba 2024
yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 4.5.
Akizungumza katika mahafali hayo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman amewakumbusha wahitimu hao kuwa maisha ya kitaaluma, na mitazamo ya maisha kwa ujumla yanabadilika kila wakati kutokana na misukumo mbalimbali ya teknolojia na mazingira.
“Hivyo, niwaombe wahitimu
wote kubadilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira na kutumia
mabadiliko hayo kama fursa ili kujiletea maendeleo yenu wenyewe, familia zenu,
jamii na taifa kwa ujumla na kuibua fursa za kujiajiri na kuwaajiri watu
wengine” amesema Mhe. Chande.
0 Comments