Na: Farida Mkongwe
Baadhi ya Waandishi walioshiriki kuandika
Kitabu cha Hayati Sokoine kiitwacho “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi
Wake” kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameeleza umuhimu wa
kitabu hicho na kusema licha ya kuzungumzia historia ya Hayati Sokoine, pia
kinatoa nafasi kwa msomaji kuielewa ipasavyo historia ya Tanzania na dhana ya
uongozi bora.
Waandishi hao akiwemo Dkt.
Emmanuel Malisa na Dkt. Onesmo Nyinondi ambao ni Wahadhiri Waandamizi kutoka
SUA wamesema Kitabu hicho kimejaa maarifa na tunu ya uongozi wa Hayati Sokoine
hivyo kuwasisitiza watanzania wote wakiwemo viongozi na vijana kujifunza kupitia historia
iliyoandikwa katika kitabu cha Hayati Sokoine.
“Umuhimu wa kitabu hiki kwa
vijana ni mkubwa kwa sababu pia kinaelezea historia ya nchi yetu kwa mfano vita
ya Uganda na Tanzania, vita ya uhujumu uchumi vijana wengi hawajui haya mambo,
kitabu kinaeleza vizuri kabila la wamasai lipo namna gani, makuzi ya kiongozi
huyu, nini kifanyike ili uwe kiongozi bora, sasa ukiangalia historia ya Hayati
Sokoine utakuta kuwa makuzi, elimu, siasa, dini na mambo mengine yamechangia
kumfanya kiongozi huyu awe mfano wa kuigwa”, amesema Dkt. Malisa.
“Wito wangu kwa viongozi ni
kupata nakala ya kitabu hiki na kukisoma kwa maana kimejaa busara na maarifa
makubwa ya kuweza kutuongoza, kitabu kimejitanabaisha kabisa na kueleza ni vipi
Hayati Sokoine amekuwa kiongozi bora na ana mchango mkubwa kwa Taifa kwa hiyo
kiongozi yeyote atakayekipata kitabu hiki na kukisoma kitamjazia ujuzi wa namna
gani anapaswa kufanya ili kuwa kiongozi bora”, amesema Dkt. Nyinondi.
Kwa upande wake Afisa Utumishi
Mkuu kutoka SUA Hilda Chigudulu amesema vijana wanapaswa kuhakikisha yale
mazuri yote yaliyofanywa na hayati Sokoine yanafanyiwa kazi katika kuleta
mabadiliko chanya katika jamii na hilo litawezekana iwapo watajifunza kupitia
historia iliyoandikwa kwenye kitabu hiki kwa sababu hawakuwepo enzi za uhai wa
Hayati Sokoine.
“Kama ambavyo amesema Mhe. Rais
Samia wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa kitabu cha Hayati Sokoine na
kuhamasisha vijana kukinunua, mimi kama kijana nimeichukua hiyo kauli na
nitahamasisha vijana wenzangu tununue ili kupata elimu na wote tuelimike ili
tuweze kuyatenda, kuyaenzi na kuyaishi matendo aliyoyafanya Hayati Sokoine”,
amesema Chigudulu.
0 Comments