Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimeahidi kuendelea kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine ambaye
alikuwa Waziri Mkuu wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea
kutoa elimu bora na kufanya tafiti zinazosaidia kuleta ufanisi na tija kwa
Taifa na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hususan watanzania waishio
vijijini.
Ahadi hiyo imetolewa Septemba 30, 2024 na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akitoa maelezo mafupi kuhusu Mradi wa Tawasifu za Viongozi wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine kiitwacho “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake” katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam.
“SUA tunajivunia mafanikio
makubwa katika kutoa mchango wa kuinua maisha ya watanzania, aidha tunaamini kuwa kupitia kitabu hiki
ambacho Chuo chetu kimepewa nafasi ya kushiriki katika uandishi wake, vizazi
vijavyo vitapata mwanga kuhusu dhamira ya Sokoine ya kuleta mabadiliko chanya
katika jamii”, amesema Prof. Chibunda.
Akizungumzia uzinduzi wa kitabu
hicho wakati akitoa salamu za familia ya Hayati Sokoine, Balozi wa Tanzania
nchini Canada Joseph Sokoine amemshukuru Rais Samia pamoja na wote walioshiriki
kufanikisha kitabu hicho kikiwemo Chuo Kikuu cha SUA na kusema kuwa hatimaye
ndoto ya karibu miaka 40 ya kusoma kitabu cha Hayati Sokoine imetimia na kwamba
kizazi cha sasa na kijacho kinaweza kupata historia ya kiongozi huyo.
Hayati Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu tarehe 13 Feb hadi 7 Nov, 1980 na mara ya pili kuanzia tarehe 24 Feb, 1983 hadi 12 April 1984 alipofariki dunia kutokana na ajali ya gari.
0 Comments