SUAMEDIA

Sekta ya Misitu kujivunia Maadhimisho ya miaka 50 ya Mafunzo ya Taaluma ya Misitu nchini


Na: Tatyana Celestine

Ukuaji wa mabadiliko chanya katika Sekta ya Misitu nchini umepelekea nchi ya Tanzania kupiga hatua ambazo zinaenda sambamba na kutoa ajira milioni 3, kuzalisha wataalamu 2,630 ambao wanasimamia misitu ndani na nje ya nchi hivyo wamewezesha kutengwa kwa hekta zaidi ya milioni 45 ya hifadhi za misitu na uanzishwaji hekta 580,000 za mashamba ya misitu ya kibiashara na kusababisha Sekta hiyo kujivunia katika Maadhimisho ya miaka 50 ya Mafunzo ya Taaluma ya Misitu nchini tangu kuanzishwa kwake 1973.

                        

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Maadhimisho hayo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Mafia  Mhe. Omary  Kipanga Octoba 1, 2024 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amebainisha kuwa Misitu nchini ina faida nyingi ambapo inachukua asilimi 55 ya ardhi kwa upande wa Tanzania Bara na kufanya misitu pekee nchini kuchangia zaidi ya asilimia nne katika pato la taifa (GDP) , upatikanaji wa maji safi, makazi na malisho ya wanyama pori , uhifadhi wa udongo, ustawi wa baioanwai, urekebishaji wa hewa ya ukaa na maendeleo ya utalii wa ikolojia.

Aidha ameongeza kuwa umuhimu wa misitu nchini uonekana katika maendeleo ya taifa, maendeleo ya viwanda katika kuongeza ajira na fursa za kibiashara nchini ingawa asilimia 20 pekee ndiyo hutumika katika mazao ya misitu hivyo kuna uhitaji wa kuangalia namna ya asilimia zilizobaki kutumika kwa kuleta tija kwa kuongeza mnyororo wa thamani na ajira katika maeneo yao huku ikiwagusa watu wenye mahitaji maalum na wanawake.

                        

Mhe. Kipanga amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa kuendelea kuongeza thamani ya bidhaa za misitu kwa kuleta teknolojia rahisi katika maeneo ya vijijini kwa wenye ujuzi na mitaji kama ilivyobainishwa na tafiti iliyofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2021 iliyoonesha ongezeko la thamani ghafi kuwa ni shilingi Trilioni 4.65 ameitaka Wizara ya Mawasiliano na Utalii, Mali Asili na Mazingira na wadau wengine wa misitu waimarishe ushirikiano na SUA kupitia Ndaki ya Misitu kuongeza ufanisi na tija katika sekta hiyo ili kufikia malengo makubwa kwa miaka 50 ijayo.

                        

Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia kwa kuithamini Taasisi ya SUA kwa kutenga muda na kushiriki katika ufunguzi wa Maonesho hayo ya kihistoria hivyo watu wote wameombwa kushiriki kikamilifu katika kujifunza na kufahamu kuhusu misitu kwani SUA  imekuwa kiongozi katika eneo la nchi za SADEC na Afrika Mashariki hivyo kupitia wiki hiyo wawe na sababu ya kufurahia pamoja na kujitathimini ili kuendelea kuwa Chuo kiongozi.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema katika miaka 50 Chuo kimekuwa na shahada mbalimbali za misitu tangu kuanzishwa kwa taaluma hiyo chuoni hapo na hakikuishia kufundisha pekee kimeendelea kuimarisha mafunzo hayo kwa vitendo ambapo kimetenga Msitu wa Mafunzo Olmotonyi Arusha wenye hekari zipatazo 800, Kitulangalo Morogoro, Msitu wa Mazumbai ambao una hekari 200 pamoja na kupanda msitu mwingine wa mafunzo Ifinga Madaba Songea  ambao unatarajiwa kuwa wa hekta elfu 10.






                            











 

Post a Comment

0 Comments