Na Gerald Lwomile
Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya
Kusini kupitia Wizara yake ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu imesema mashirikiano
katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu baina ya Tanzania na Afrika ya Kusini yataleta
maendeleo kati ya pande hizo mbili.
Hayo yamesemwa Oktoba 30, 2024 na
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Afrika ya Kusini Dkt.
Bonginkosi “Blade” Nzimande wakati akizungumza na viongozi na menejimenti ya
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo alipofanya ziara yake ya siku moja chuoni
hapo.
Dkt. Nzimande amesema ni muhimu
kuwepo kwa ushirikiano kati ya nchi yake na SUA katika maeneo mbalimbali kama
Utafiti, Teknolojia na Program za kubalishana uzoefu kwa wanafunzi na wataalamu
ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo katika sekta ya kilimo na kuleta
maendeleo kwa watu wake.
Waziri huyo wa Sayansi,
Teknolojia na Ubunifu amesema endapo nchi hizi mbili zitafanya tafiti
mbalimbali kwa pamoja zinaweza kuja na matokeo ambayo si tu yatazisadia nchi
hizo mbili bali Afrika kwa ujumla.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Afrika
ya Kusini itaangalia uwezekano wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi
kutoka Afrika ya Kusini kuja kusoma katika vyuo vilivyopo Tanzania ikiwa ni
pamoja na SUA.
Awali akijibu hoja zilizoibuliwa
na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika ya Kusini na
Bi. Linaliwe Gama na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo Bi. Karabo Mlambo waliotaka
kujua kwanini hawaoni wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini wanaosoma SUA, Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amesema SUA
imekuwa ikipokea wanafunzi kutoka nchi za Botswana, Lesoto, Mozambique na
maeneo mengi yaliyoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Amesema ni matumaini yao kuwa
katika siku za usoni watapata wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini na hasa kama
wataondoa mtazamo hasi wa elimu
inayotolewa katika vyuo vya Tanzania ikiwa ni pamoja na SUA kwani chuo hicho kinafanya
vizuri kwa kufundisha na kutoa wataalamu mbalimbali katika maeneo mengine ya
Afrika.
Amesema endapo kutakuwa na
ufadhili unaotolewa kwa wanafunzi kutoka Afrika ya Kusini watakuja na kupata
elimu na ujuzi bora na huenda hata wakatamani kubaki nchini kutokana na kuwepo
kwa mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na amani na utulivu uliopo.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya
Sayansi na Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini
Prof. Ladislaus Mnyone amesema endapo ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na
Afrika ya Kusini katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu utaboreshwa basi utaleta
maendeleo kwa pande zote mbili
Amesema wao kama Wizara
wamefurahishwa na ziara hiyo ya Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka
Jamhuri ya Afrika ya Kusini na kuwa itaimarisha ushirikiano baina ya pande hizo
mbili.
0 Comments