SUAMEDIA

Rais Samia azindua Kitabu cha Hayati Sokoine, awataka vijana kukisoma ili wapate mafunzo ya uongozi

 

Na: Farida Mkongwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua kitabu cha Hayati Edward Moringe Sokoine kiitwacho “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake” na kuwataka viongozi wote wakiwemo vijana kukisoma kitabu hicho ili wapate mafunzo ya uaminifu, nidhamu na uchapakazi ambayo ni alama iliyoachwa na Hayati Sokoine.



Rais Samia ametoa kauli hiyo Septemba 30, 2024 wakati akizindua kitabu hicho katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam na kusema Hayati Sokoine alikuwa ni Kiongozi mwenye nidhamu, mzalendo, mwaminifu, muadilifu, mchapakazi, aliyedumisha mila na mpenda haki hivyo watanzania hawana budi kusoma kitabu hicho ili waweze kuiga misingi ya uongozi kutoka kwa Hayati Sokoine.

Rais Samia amesema kwa mujibu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 asilimia 81.21 ya watanzania wapo chini ya umri wa miaka 40 kwa maana kwamba kati ya kila watanzania  5 waliopo sasa ni mmoja tu ndiyo alikuwa hai wakati Sokoine anafariki dunia mwaka 1984, hivyo ni muhimu kutunza na kusimulia vizuri kumbukumbu za shujaa huyo ili vijana waweze kusoma na kujifunza  uongozi kupitia historia yake.

“Kitabu hiki tunachokizindua leo sio tu kinaonesha maisha ya kiongozi huyu mashuhuri bali pia fikra, mawazo yake, kazi zake, changamoto alizokutana nazo, na jinsi alivyojenga misingi imara ambayo nchi yetu inaendelea kunufaika nayo hadi sasa”, amesema Mhe. Samia.


Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewasihi watanzania na wadau wote wa maendeleo kusoma kitabu cha Hayati Sokoine ili wapate mafundisho na kuyatumia katika kuboresha utendaji wao wa kazi na kuleta maendeleo yatakayoimarisha Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema ili kuendelea kumuenzi na kukumbuka fikra za Hayati Sokoine, tangu mwaka 1992 Chuo hicho kimekuwa kikiandaa kila mwaka Mhadhara wa Kumbukizi ya Sokoine ambapo April 8, 2024 Chuo kilifanya Mhadhara wa Kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Sokoine ambao ulienda sambamba na hafla ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SUA.

Kitabu  cha “Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake“ kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  na Taasisi ya UONGOZI ambacho kinaangazia safari ya  Kiongozi huyo kuanzia Makuzi yake katika jamii ya Kimasai hadi nyadhifa za Uongozi wake ikiwemo Waziri Mkuu kina Sura 14, Kurasa 499 na jumla ya watoa taarifa 57 walihojiwa katika kufanikisha uandishi wa kitabu hicho.







 







Post a Comment

0 Comments