Wazazi na walezi wenye vijana
ambao wanataka kujiunga na vyuo vikuu lakini wanaona vijana wao wana changamoto
katika masuala ya matumizi ya lugha wametakiwa kufika katika Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kutatua changamoto hizo kupitia Idara ya Taaluma
za Lugha iliyopo Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia chuoni hapo.
Kauli hiyo imetolewa na Mhadhiri
Mwandamizi kutoka Idara hiyo Dkt. Job Mwakapina wakati akizungumza na SUA Media
kwenye Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya
Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Dkt. Mwakapina amesema katika
Idara yao kuna Kituo cha Lugha za Kiafrika na za Kimataifa ambacho kinatoa
huduma mbalimbali zikiwemo kozi za muda mfupi za miezi mitatu au minne za lugha
ya kiingereza na kiswahili na pia wanashirikiana na vyuo vingine duniani kutoa
mafunzo ya muda mfupi kwa lugha za kijerumani, kiarabu na kifaransa.
”Pia Kituo hiki kinafanya tafiti katika
lugha hizi ambazo nimezisema hivyo nitoe wito tu kwa wazazi na walezi hasa
katika kipindi hiki ambapo vijana wanasubiri kwenda chuoni kama kijana hayupo
vizuri kwenye lugha basi mlete sisi tutamuandaa vizuri ataenda chuoni akiwa
safi”, amesema Dkt. Mwakapina.
Huduma nyingine zinazotolewa na
kituo hicho ni kutafsiri maandiko, kutoa mafunzo ya maandalizi kwa ajili ya
mitihani ya kimataifa ya kiingereza, kutoa huduma ya ukarimani kutoka Kiswahili
kwenda kiingereza au kutoka kiingereza kwenda kifaransa.
“Hicho ni kituo kimoja lakini
kituo cha pili ni cha mambo ya kijinsia ambacho kinatoa huduma ya kujenga uelewa
kwa jamii inayotuzunguka juu ya mambo ya kijinsia, kufanya tafiti mbalimba
katika maeneo ya jinsia na kutoa mafunzo ya muda mfupi yanayohusiana na
jinsia”, amesema Dkt. Mwakapina.
0 Comments