Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Imeshauriwa kuwa uwekezaji katika
sekta ya kilimo ujikite zaidi katika kuangalia namna ya kuboresha mbinu
mbalimbali za ugani na teknolojia za kisasa ili kuwasaidia maafisa ugani kufikisha
taarifa bora na za kisasa kwa wakulima vizuri na kuinua tija.
1. Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Catherine Msuya akichangia mada kwenye japo akieleza nafasi ya ugani kwenye uwekezaji wa Kilimo.
Ushauri huoumetolewa leo jijini
Dodoma na Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) na Mhadhiri kutoka
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Catherine Msuya wakati wa kongamano la
kimataifa lililolenga kuangalia mchango wa uwekezaji katika sekta ya kilimo
ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo
china na Marekani lililofanyika Jijini Dodoma kwenye maonesho ya Kitaifa ya
wakulima nanenane.
“Maafisa ugani bado wamekuwa
wakiendelea kutumika njia za zamani japokuwa zipo jitihada zinazoendelea za
kufanya wanafunzi ambao wapo vyuoni kujifunza mbinu za kisasa, lakini vipi wale
wagani ambao tayari kundi kubwa lipo kule likifanya kazi wanajifunza wapi,hivyo
ipo haja ya kuwekeza katika kuwapa elimu na maarifa ya hayo mapya na ya kisasa
yanayokuja” alibainisha Prof. Catherine.
Aliongeza “Unakuta Mgani
amemshauri mkulima kutumia mbegu flani ambayo ilikuwa ikitumika siku zote na
ikifanya vizuri lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ile mbegu haifanyi
vizuri mkulima mfugaji au mvuvi anakuwa anasahau kwamba kuna mabadiliko ya
tabia nchi hivyo lawama zinakuwa kwa afisa ugani”.
Awali akifungua kongamano hilo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo
amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kilimo ili kuhakikisha tija inaongezeka hivyo amewataka
wakulima kutumia maarifa mbalimbali wanayopewa ili waweze kufikia lengo lao na
la Taifa.
1. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akifungua Kongamano hilo la Kitaifa la Uwekezaji.
“Natoa wito kwa sisi viongozi na
watumishi wenye dhamana kusaidia wakulima tuendelee kuweka mazingira mazuri ya
biashara na uwekezaji ili wakulima wetu wanapolima wahakikishe wanapata nafasi
ya kuuza mazao yao kwa njia ambayo haina vikwazo ili wabadili mazao yao kuwa fedha
hiyo ndiyo njia nzuri ya kuongeza kipato na kuondoa umaskini”, alisema Prof
Kitila.
Aidha ametoa wito kwa wawekezaji
kutoka nje kuja kuwekeza katika kilimo hususani kwenye viwanda kwasababu lengo
ni kuongeza thamani mazao ya kilimo Mifugo, Uvuvi, Misitu na Madini ili kuweza
kusafilisha bidhaa zilizoongezeka thamani na kupata fedha nyingi zaidi.
Aidha kwa upande wake Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amesema kuwa Kongamano ni nyezo muhimu kwasababu
linawafungua watu macho kujua yale ambayo hawakuwa wakiyajua na linasaidia
kutoa nafasi ya kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa changamoto kwa pamoja
kupitia majadiliano.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akitoa salamu zake kwa washiriki wa Kongamano hilo la Kimataifa kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane Kitaifa Jijini Dodoma.
“Kuna mengi ambayo tukienda kukaa
tukayatafakari na mengine kutengenezewa mpango kabisa mimi naamini yatawaongezea
sana maarifa mapya kwa Wananchi wetu kutoka hapo walipo na kupiga hatua moja
mbele”, alisema mhe Pinda.
Maafisa Ugani hao kupitia chama
chao cha maafisa ugani Tanzania (TSAEE) wanakutaka kwenye maonesho hayo ya
Kitaifa ya nanenanen Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali mpya
na za kisasa zilizopo ili kuwajengea maarifa mapya ambayo yatawasaidia katika
kutatua changamoto mbalimbali za wakulima kwenye maeneo wanayotoka nchi nzima.
0 Comments