Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeiomba Serikali ifikirie namna ya kuwawezesha wataalam wa utafiti nchini kwa kuwapa ufadhili ili waweze kufanya tafiti nyingi zenye maslahi na manufaa kwa taifa.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa
Chuo hicho Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Jaji Joseph
Sinde Warioba wakati akitoa salaam za Chuo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Jengo Mtambuala la
Mafunzo Agosti 6, 2024 katika Kampasi ya Edward Moringe Sokoine mjini Morogoro.
Mhe. Jaji Warioba amesema watafiti
pamoja na kufanya kazi nzuri katika tafiti zao wanakabiliwa na changamoto ya
kupata ufadhili wa ndani hali inayowapa ugumu kufanya tafiti zao katika maeneo
mbalimbali nchini kwa kuwa wafadhili kutoka nje wana masharti na maeneo yao wanayotaka
yafanyiwe utafiti.
“Sehemu kubwa ya utafiti
inafadhiliwa na watu wa nje, asilimia 92 ya fedha zinazotumika kwenye utafiti
zinatoka kwa wafadhili wa nje, fedha zetu ni
asilimia 8 tu, lakini wafadhili kutoka nje wana maeneo yao hivyo sisi
tukitaka kufanya utafiti kwa maeneo ya humu ndani kwa maana ya Tanzania hatuna
uwezo”, amesema Mhe. Jaji Warioba
Aidha Mhe. Warioba amezungumzia
umuhimu wa tafiti zinazofanywa na watafiti mbalimbali kufika kwa walengwa ili
matunda ya matokeo ya tafiti hizo yaweze kuinufaisha jamii na taifa kwa ujumla.
“Matokeo ya utafiti wakati
mwingine yanabaki hapa hapa nadhani ifike wakati tuanze kuweka utaratibu ambao
matokeo ya utafiti unaotokea hapa yaweze kufika katika vitengo vinavyohusika
ambapo itasaidia katika kuandaa Sera na kufanya mipango ya maendeleo”, amesema Mhe.
Jaji Warioba.
0 Comments