Na: Farida Mkongwe
Wananchi, makampuni na watu
binafsi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa ya biashara ya Kaboni
ambayo inalenga kupunguza gesi joto na kuwajengea wananchi maendeleo endelevu wakiwemo
wakulima na wafanyabiashara.
Wito huo umetolewa Agosti 3, 2024
na Mhadhiri Mwandamizi na Msaidizi wa Mratibu wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji
wa Kaboni nchini kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Dkt. Deo
Shirima wakati akizungumza na SUA Media katika banda la Chuo hicho kwenye Maonesho ya Nane nane Kanda ya
Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini
Morogoro.
“Kama alivyosema Rais Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan na kauli mbiu ya nishati safi ya kupikia, biashara ya
kaboni inatoa fursa kama motisha kwamba tunapofikia lengo la nishati safi kwa
maana tunabadilishana nishati ile iliyokuwa inachafua mazingira kwenda kwenye
nishati safi ya kupikia lakini wakati huo huo tunapata faida ya ziada au
motisha kwa kupitia biashara ya kaboni”, amesema Dkt. Shirima
Dkt. Shirima ametoa wito kwa
makampuni ambayo yanajikita kwenye kauli mbiu hiyo ya Serikali ya nishati safi
ya kupikia yafikirie kuongeza eneo la biashara ya kaboni katika miradi yao na
pia kwenye masuala ya mazingira, kilimo na biashara ambayo inaweza kuwa fursa
nzuri ya kusaidia kuongeza motisha kwa kutunza mazingira na kufaidika na
biashara ya kaboni kama utasajili kuwa sehemu ya biashara hiyo.
“Mpaka sasa Kituo kimesha sajili
miradi ya kaboni zaidi ya 50 na miradi hiyo ipo katika sekta mbalimbali, miradi
mitatu tayari imeshaanza kufanya kazi na kutoa faida na wananchi wameshaanza
kunufaika, unaweza kufanya miradi hii katika sekta mbalimbali mojawapo ambayo
watu wanaweza kuwekeza ni kwenye sekta ya misitu ambayo mpaka sasa tuna hekta
takribani milioni 19 ambazo wameshajitokeza wawekezaji wanataka kuwekeza”,
amesema Dkt. Shirima.
Amesema miradi hiyo inaweza
kusajiliwa kwa kuzingatia kanuni inayosimamia uwekezaji wa miradi ya kaboni
nchini na kwamba watu wanaweza kujiunga kama kikundi wakajisali kwenye biashara
ya kaboni na kitu kikubwa zaidi na kizuri ambacho kimewekwa kwenye kanuni ni
kwamba ni lazima kuona namna gani wale wanaozunguka rasilimali za hapa nchini
mfano misitu, nishati, kilimo wanafaidika na biashara yenyewe..
“Chimbuko la biashara hii ni kama
tunavyofahamu kumekuwa na ongezeko la gesi joto duniani na hivyo mataifa
ulimwenguni kote yakataka kuhakikisha tunapunguza ongezeko hilo, sasa ili
kufikia azma hiyo ndiyo kukawa na utaratibu wa kuzitaka nchi ambazo zimeendelea
na kuzalisha gesi joto kwa wingi zione namna gani ya kuweza kuingia kwenye
mfumo wa kimasoko ambao utafanya wale watakaokupunguza gesi joto waweze kupata
motisha na hivyo kutengeza fursa ya kibiashara”, amesema Mhadhiri huyo.
PICHA NA TATYANA CELESTINE
0 Comments