Na: Farida Mkongwe
Wafugaji
nchini wametakiwa kutumia teknolojia mpya ya uhimilishaji wa kuku inayopatikana
katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) ambayo inatoa nafasi kwa mfugaji kuchagua aina ya mbegu bora ya kuku
anaotaka kufuga ambao watakuwa na uzalishaji utakao mletea faida.
Teknolojia
hiyo imewekwa bayana na Afisa Mifugo Mwandamizi Bi. Enesa Mlay kutoka Ndaki ya
Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya SUA wakati akizungumzia namna ya kupata
mbegu bora za kuku wa asili katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Akizungumzia namna teknolojia
hiyo inavyofanya kazi Bi. Enesa amesema kinachofanyika katika uhimilishaji ni
kuwa kunakuwa na majogoo na majike ambapo inatolewa mbegu kwa majogoo na
kuiweka kwenye njia ya uzalishaji wa majike hali inamuwezesha mfugaji kupata
vifaranga kutokana na mbegu aliyoichagua.
“Sasa hivi wafugaji wetu
tunawaelimisha kuwa wasikae na majogoo na matetea ambao ni ndugu au ni wa ukoo
mmoja kwa sababu wakipandana wakati ni ndugu wakati mwingine jogoo anampanda
tetea ambaye ni mtoto wake au dada yake hii inaleta changamoto katika kupata kuku wenye ubora hivyo njia hii
ya uhimilishaji ni teknolojia sahihi ya kuondoa changamoto hii”, amesema Afisa
Mifugo huyo.
Amezitaja changamoto za kuku
kupandana wakiwa ndugu au ukoo mmoja kuwa ni kushindwa kupata mbegu bora kwa
sababu kuku watakaototolewa watakuwa wadogo kwa umbo, kupata kuku walemavu na
dhaifu kiafya pamoja na kukosa muendelezo wa mbegu bora kwa siku zijazo na
hivyo kupoteza wazazi bora katika ufugaji wako.
PICHA NA TATYANA CELESTINE
0 Comments