Na: Winfrida Nicolaus
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kupitia Ndaki ya Kilimo, Idara ya Mimea,
Vipando na Mazao ya Bustani imekuja na Kliniki ya Mimea kwa ajili ya kuwasaidia
wakulima kote nchini kuweza kutambua ubora wa mbegu na aina ya ugonjwa katika mazao
yao na namna ya kudhibiti magonjwa hayo kwa kutumia vifaa vyenye ubora na vya
kisasa toka kwenye Kliniki hiyo.
Amebainisha
hayo Bw. Isack Kazosi Afisa Kilimo kutoka Idara ya Mimea, Vipando na Mazao ya
Bustani, Kitengo cha Kliniki ya Mimea SUA wakati akizungumza na SUAMEDIA katika
Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi Kanda ya Mashariki kwenye Viwanja vya
Mwalimu Julius Nyerere mjini Morogoro.
Amesema wakulima
walio wengi wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa
katika uzalishaji na ukuzaji wa mazao shambani na wanakosa namna nzuri ya kudhibiti
changamoto hizo hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutembelea Banda la SUA kwenye
maonesho hayo ili kuweza kukutana na wataalam katika Kliniki hiyo kwa elimu na ushauri
juu ya jinsi ya kutambua tatizo kwenye
mmea na namna ya kulidhibiti tatizo hilo.
“Tunazo
mbinu za kutambua ubora wa mbegu hivyo mkulima anaweza kuja na mbegu zake alizo
nazo ili kuweza kujua ubora wa mbegu hizo lakini pia endapo kutaonekana na
vimelea vitakavyoleta changamoto kwenye uzalishaji na kushindwa kupata mazao
stahiki atapata ushauri wa kumuwezesha kupata mazao yenye tija”, amesema Bw.
Kazosi.
Aidha Bw.
Kazosi amesema kwa yule mkulima ambaye ana mazao tayari shambani na
yameshambuliwa na magonjwa na kushindwa kujua namna sahihi ya kudhibiti
magonjwa hayo apeleke sampuli kutoka shambani ili iangaliwe na kuweza kutambua
aina ya ugonjwa unaosumbua mazao yake na kupatiwa ushauri wa namna sahihi ya
kudhibiti .
Maonesho
ya Nanenane mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa
Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”
0 Comments