SUAMEDIA

Wataalamu wa APOPO (SUA) kwenda Uturuki kupata mafunzo zaidi ya panya kuokoa maisha ya binadamu

 Na: Farida Mkongwe

Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia APOPO ambayo inashughulika na kuokoa maisha ya watu hivi karibuni wanatarajia kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kupata mafunzo zaidi ya kutumia Panya katika kuokoa maisha ya wahanga wa majanga mbalimbali yanayotokana na tetemeko la ardhi au majengo kuporomoka.

                                    

Hayo yamebainishwa Agosti 4, 2024 na Mkufunzi wa Panya kutoka APOPO SUA Abouswai Msuya wakati akizungumzia jinsi panya hao wanavyotumika kuokoa maisha ya wahanga wa kufukiwa ardhini pamoja na kusaidia katika udhibiti wa utoroshwaji wa  nyara za Serikali kwenye makontena alipozungumza na SUA Media katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mjini Morogoro.

                                



“Tayari tumepata wadhamini kule Uturuki na wangependa tuweke kituo kule ili kazi iwe rahisi na kuendelea kupanua wigo, hii itasaidia kutangaza kwenye mataifa mengine kuhusu hii teknolojia ambayo inafanyika hapa APOPO na mataifa mengi yataweza kunufaika na teknolojia hii”, amesema Mkufunzi huyo.

Amesema kwa duniani, Tanzania kupitia SUA  ndiyo nchi pekee inayojihusisha na mambo ya uokoaji wa maisha ya wahanga wanaopatwa na majanga kwa kutumia panya hivyo kupatikana kwa fursa hiyo ya kwenda kufanya mafunzo nchini Uturuki kutasaidia mataifa mengine kufahamu kazi inayofanywa na panya hao na kuwatumia pale inapohitajika kufanya hivyo.

Akizungumzia kuhusu Panya wanaosaidia katika udhibiti wa utoroshwaji wa  nyara za Serikali, Mkufunzi huyo wa Panya amesema kwa sasa timu ya APOPO ipo bandarini jijini Dar es Salaam ikiendelea na zoezi la kuhakikisha kuwa wanadhibiti utoroshwaji wa nyara za Serikali katika makontena yote yaliyopo bandarini.

“Zipo ishara ambazo tunawasiliana na panya anapogundua kuwa humo ndani kuna nyara, panya akishagundua mle ndani kuna hizo nyara baada ya kunusa, yule panya shingoni kuna kifaa atakuwa amevishwa kitaalamu kinaitwa Vest atakivuta kile kifaa kitendo cha kukivuta kile kifaa kitatoa sauti sisi tutagonga kengele kumjulisha aje achukue zawadi hapo ina maana hilo kontena lina nyara za Serikali, ikiwa hakuna nyara za Serikali basi yule panya hatashughulika kuvuta hicho kifaa alichofungwa shingoni”.

“Panya hawa tunawafundisha toka hatua za awali wakiwa watoto lakini baadaye wakishafahamu kila kitu basi tunawapeleka bandarini kwa ajili ya kugundua yale makontena ambayo yana hizo nyara za Serikali na kwa sasa nyara wanazoweza kugundua ni kama pembe za ndovu, Kakakuona na miti ya mpingo”, amesema Abouswai.

 







Post a Comment

0 Comments